Mchekeshaji na muigizaji maarufu wa Kenya Ithagu Kibicho almaarufu Henry Desagu amekanusha madai ya kukumbwa na msongo wa mawazo.
Hii ni baada ya ripoti katika mitandao ya kijamii kudai kuwa msanii huyo anayeishi Mwihoko alipatikana katika hali ya kusikitisha huku akirandaranda Thika Road.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini , aliweka wazi kuwa yuko sawa na hapitii matatizo ya kisaikolojia kama ilivyoripotiwa.
“Haya
mambo ni mtu aliandika. Unapata wakati tuko kwenye mitandao ya kijamii, watu
wako tayari sana kuchukua habari mbaya. Lakini ukiangalia Desagu, niko salama
salmini. Sina bugdha, sina kutekelezeka figo, yaani sina mpwito pwito wowote.
Niko salama kabisa,” Desagu alisema.
Mchekeshaji huyo kijana hata hivyo alikiri kwamba pia anapitia hali ngumu ya maisha katika nyakati ngumu za kiuchumi za sasa.
Huku akizungumzia picha zilizovuma ambazo zilisemekana kuwa zake anatembea kwenye Barabara ya Thika, alisema, “Kama nimekuwa Barabara ya Thika, nimekuwa tu kwa gari. Lakini mimi ni mtu wa sherehe. Mimi ni mtu wa watu. Tuseme kama mimi ni msanii, hakuna mahali huwa siingii.”
Desagu alidai kuwa mtu aliyeeneza madai ya yeye kupatikana katika hali ya kusikitisha alikuwa akitafuta kiki tu kwa lengo la kuwa kwenye habari.
“Mimi ni Mkenya wa kawaida, nitaenda huko nje. Kama ni kwa kujiburudisha nitaenda kama wengine, kama watu huzima ata mimi nitazima sio eti yangu ni maalum. Kwa hiyo, ukiwa katika ile hali, mtu anaweza kuja akuone. Msanii kuna mambo mengi unapitia, na sio kila kitu unapata lazima kiwe cha usanii, inaweza kuwa mambo ya familia ama marafiki. Lakini mtu akienda achukue hiyo maneno, unajua hakuna vile utakuja upinge useme haikuwa hivyo. Sasa unaacha iende vile alisema,” alisema.
Aidha,
msanii huyo alionekana kupuuza shinikizo la yeye kupelekwa katika hospitali ya
kiakili ya Mathare, akibainisha kuwa yuko sawa kiakili.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mchekeshaji huyo mzaliwa wa Nakuru kudaiwa kuokolewa na wasamaria wema akiwa katika hali mbaya kando ya barabara ya Thika.