MFANYIBIASHARA na mfanyikazi wa kanisani kutoka jijini Nakuru, Elias Njeru kwa mara ya kwanza amezungumza kuhusu mzozo uliotokea baina yake na mpenzi wake wiki mbili zilizopita.
Akizungumza na mtengeneza maudhui Metha ya Kagoni kupitia chaneli yake ya YouTube, Njeru alisimulia kwamb kilichojiri na kuwa gumzo nchini kote kwenye mitandao ya kijamii kilichipuka kutokana na mzozo wa kimapenzi.
Mfanyibiashara huyo alifichua kwamba ana mke mmoja jijini Nairobi na mpaka kutokea kwa mzozo huo, alikuwa amepata mpenzi mwingine katika jiji la Nakuru vile vile.
“Jambo la ajabu ni kwamba niliona wakati bado niko shuleni; chuo kikuu. Niko na mke mmoja Nairobi na nilikuwa nimepata mke mwingine Nakuru. Wa Nairobi ndiye wa kwanza na tulioana tukiwa chuo kikuu, anaitwa Wairimu,” Njeru alifunguka.
Njeru alisema kwamba baada ya kumaliza shule, walioana na kuendelea kuishi pamoja na mpaka sasa uhusiano wao una miaka 12 na watoto 3, na kwamba mwaka ujao wanapanga kufanya harusi.
Lakini je, Njeru alijipata aje katika uhusiano wa pili na mwanamke wa Nakuru?
Kwa mujibu wake, uhusiano wake na mke wa kwanza wa Nairobi haukuwa na shida yoyote kupelekea kutafuta familia ya pili jijini Nakuru.
Mwanamke wa Nakuru – Florence – ni mtu waliyeanza kufanya kazi na yeye na katika hizo harakati, uhusiano ukaota na wakapata mtoto pamoja.
“Tumekuwa na Florence takribani miaka 3 yenye mke wa kwanza [Wairimu] hakujua kwa sababu singetaka ajue mapema hivyo. Kwangu nilikuwa nimepanga ajue baadae wakati labda watoto wamekuwa wakubwa.”
“Florence si mtu mbaya, na ndio maana niliona ni mtu tunaweza ishi na kusaidia na yeye na tena kuna watoto wamekuja, nikaona tuishi na yeye tu,” Njeru aliongeza.
Njeru alisema kwamba mke wa kwanza hakuwahi jua kwamba ana mke wa pili hadi pale mke wa pili mwenyewe alipoamua kutafuta namba yake na kumueleza kwamba yeye pia ni mke mwenza.
“Kuna kitu Fulani kuhusu wanawake na kujidhibiti kihisia. Florence kuna mahali alishjindwa kujizuia na akamwambia Wairimu. Alipata namba ya Wairimu na jambo la kusikitisha ni kwamba alipata kutoka kwa rafiki. Siku moja akajipata amempigia Wairimu na kumwambia kwamba ‘jua na sisi tuko na mtoto na Elias’. Wairimu aliniuliza, na haya yote yalitokea huu mwaka kama miezi minne iliyopita,” alisema.
“Wairimu aliniuliza,
sikukataa. Nilimwambia ni ukweli na ‘samahani sana kwamba ilinibidi kufanya
vile’. Nikamwambia itaishia hapo hatanisikia tena kwingine na nikamuuliza kama
inawezekana tuendelee sote pamoja. Lakini muda wote huu hakuwa amekubali,
amekuwa akiliombea suala hilo sana,” Njeru alisimulia zaidi.