Staa wa Bongo, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amefichua kuwa alilipwa $150,000 (Ksh19.4m) kutumbuiza jijini Nairobi, Kenya mnamo Desemba 7.
Diamond alikuwa miongoni mwa wasanii wakubwa waliotarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha la Furaha katika Klabu ya Polo, Nairobi wikendi iliyopita. Bosi huyo wa WCB hata hivyo hakupanda jukwaani kama ilivyotarajiwa na kuwaacha mashabiki wake na washiriki wengine wa tamasha hilo wakiwa na ghadhabu kubwa.
Katika taarifa ya video aliyoitoa siku ya Jumanne, akielezea sababu ya kutotumbuiza, mwimbaji huyo alithibitisha kuwa alilipwa mamilioni ya pesa kutumbuiza lakini alichoshwa na jinsi tukio hilo lilivyotokea kuwa na kumfanya asitumbuize jinsi alivyopanga.
“Mimi nimelipwa pale, nimelipwa dola laki moja na hamsini. Nafikiria hiyo ni milioni 400 za Tanzania,” Diamond alisema.
Bosi huyo wa WCB aliendelea kupuuzilia mbali madai ya kujilazimisha kutumbuiza jukwaani kabla ya wasanii wengine, kama ilivyodaiwa awali na baadhi ya wasanii wa Kenya.
Aidha, alibainisha kuwa alikuwa tayari kutumbuiza wakati ambao walikuwa wamekubaliana na mwandaaji, lakini kukawa na ucheleweshaji uliomfanya aondoke licha ya kulipwa.
“Wewe si ushanilipa mimi. Nitasubiri mpaka uwe tayari. Nitaangalia tu muda wangu, nikiona muda huu sio wangu tena kwenda steji, naondoka naenda zangu. Mambo ya eti mimi niliforci, sijui nililazimisha, sifanyi hayo. Wewe ushanilipa, mimi nasubiri muda wangu, ukishindwa kunipandisha katika tarehe tuliyokubaliana, naondoka na hela zako. Sina muda wa kulazimisha ama kukataza mtu kupanda kwenye steji,” alisema.
Diamond alilalamika kwamba hakukuwa na mpangilio mzuri wa hafla hiyo, akidai kuwa machafuko mengi yalizuka na alisubiri kwa zaidi ya masaa matatu bila kupandishwa jukwaani.
Alidai kuwa alifahamu kuwa angetumbuiza wa mwisho kwenye hafla hiyo, lakini mwandaaji alishindwa kumpandisha jukwaani kwa muda uliokubaliwa.
Licha ya tukio hilo la kusikitisha, staa huyo wa bongo fleva alidokeza kuwa yuko tayari kutumbuiza nchini Kenya tena wakati kutakuwa na mpangilio mzuri.