Mbwa aliyefahamika mno katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani kwa jina Chloe ameripotiwa kuaga dunia. Kifo cha Chloe kilitukia mchana wa Disemba 9, kufuatia wiki kadhaa ya udhaifu wa kiafya.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kupitia anwani yake kwenye mtandao wa X, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika makao yake makuu waliaga Chloe mapema mwanzoni mwa mwezi huu.
Mbwa huyo alisifika kwa kuwa sehemu muhimu ya matibabu ya hali ya akili yanayokusudiwa kupunguza au kuponya magonjwa.
Umoja wa Mataifa umesifia utendakazi wa Chloe kwa kuleta tabasamu kwa kila mmoja aliyekutana naye katika Umoja wa Mataifa. UN imesema kwamba alileta furaha na huruma kila mahali alipoenda.
“Baada ya kuleta tabasamu nyingi na faraja isiyoisha, mapema mwezi huu,wafanyakazi katika UNHQ huko New York waliaga Chloe – mbwa wetu mpendwa wa tiba.” Umoja wa Mataifa uliandika kwenye anwani yake ya mtandao wa X.
Mbwa huyo, ametumika katika hafla mbali mbali za uhamasisho kwa binadamu katika maswala kadha wa kadha ikiwemo utunzaji wa maji, hafla za kuadhimisha siku ya watoto, hafla za uhamasisho wa afya bora pamoja na hafla ya kusherehekea uzinduzi wa Water Action Decade uliofanyika mwezi Machi mwaka wa 2018.
Kwa kawaida mbwa wa aina ya Bulldog huishi kwa wastani wa miaka kati ya 8 na 10 ila Chloe aliishi kwa takribani miaka 13 duniani. Chloe alizaliwa mnamo Agosti 9, 2011.
Aidha kupitia anwani ya ‘Chloe, The UN Therapy Dog’ kwenye mtandao wa facebook, ambapo kifo cha mbwa huyo kilitangazwa mnamo Disemba 9, iliarifiwa kwamba Chloe alifahamu kukaribia kwa mauti yake kutokana na hali yake ya kiafya aliyokuwa nayo katika wiki kadhaa.
Hata hivyo anwani hiyo, ilielezea risala zake za rambi rambi kwa marafiki, familia ,wafanyakazi na mashabiki wa Chloe kwa upendo waliomwonyesha katika aushi yake upendo uliotajwa kumfanya kusidhi miaka mingi kinyume na wastani wa mbwa aina ya Bulldog.
“Natoa shukrani zangu za dhati kwa marafiki wake, familia, wafanyakazi
wenza na mashabiki kwa mapenzi mlimpa. Nimeshawishika upendo wenu ulichagua
pakubwa maisha yake marefu yenye furaha.” Ujumbe huo ulisema kwenye
Facebook.
Chloe aliishi zaidi ya nusu ya maisha yake
katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa akisaidia katika matibabu.