Mwimbaji maarufu wa nyimbo za mtani Stoopid Boy amefunguka kuhusu baadhi ya
masaibu ya kimahusiano yaliyompata miaka kadhaa iliyopita.
Akizungumza katika mahojiano na Oga Obinna, mwimbaji huyo mwenye kipaji ambaye ametangaza waziwazi kutowapenda wanawake tena alifichua kuwa mkewe alimwacha takriban miaka mitano iliyopita.
Stoopid Boy alisimulia jinsi mwanamke ambaye alikuwa na watoto wawili alitoroka baada ya yeye kufilisika, na kuacha familia yao changa ikiwa imesambaratika.
“Bibi yangu alitoroka na kila kitu changu na akaniachia Pipi na Dior. Niko na watoto wawili. Patricia na Dior ni kijana wangu na msichana wangu. Na mama yao alitoroka, na ndio maana huwa nasema sina mdem siku hizi. Mimi nilikasirika sana na madem wote. Sipendangi ata kuskia stori za madem mimi,” Stoopid alisema.
Rapa huyo alifichua kuwa mmoja wa watoto wake kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa mama yake ilhali mtoto mwingine yuko na mzazi mwenzake.
“Pipi alirushiwa mokoro wangu huko. Ako kwetu. Pipi ako daraja la kwanza. Dior sijui mahali mamake alienda na yeye. Sijui mahali yeye hukuwa,” alisema.
“Ni kama (mzazi mwenza) alinipenda wakati nilikuwa na pesa kisha nikasota. Ata sikuwa naimba wakati huo. Nilikuwa nauza steam, na napimisha chuma, nilikuwa na baze yangu nikaibiwa mkokoteni na kila kitu nikaambiwa nijilee,” aliongeza.
Akizungumzia ni kwa nini mzazi mwenzake alimuacha, Stoopid Boy alisema, “Aliniacha juu ya mihadarati, hata sio kusota sanasana. Nilikuwa natumia madawa sana, lakini nilikuja nikaziacha. Nilikuwa nazitoa kwa daktari ndio nitulie tu.”
Mwimbaji huyo kijana hata hivyo alidokeza kuwa atakuwa tayari kumsamehe mpenzi wake wa zamani ikiwa ataamua kurudi.
“Mdem wangu alipata kazi tukakosana. Ni kama alioleka huko. Mahali tu ako, anirudishie mtoto wangu yeye atembeze tu huko kando. Akirudi nitamsamehe tu, siwezi weka za moyoni mimi sio mdem. Mimi napenda watoto, siwezi nikasema nampenda mama yao. Nilikuwa nampenda. Huyo msichana alinisambaratisha. Aliniacha kitu kama 2019," alisema.
Stoopid Boy alipata umaarufu zaidi mwaka
jana baada ya kuachia wimbo ‘G-bag na jug’ ambao sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni
6 kwenye YouTube.