Akothee afunguka jinsi alivyofukuzwa na aliyekuwa mumewe mzungu akiwa mjamzito

Akothee amesema mume huyo wake wa zamani alidai kuwa hakuwa tayari kuwa na mke

Muhtasari

•Akothee amesema alikuwa na ujauzito wa miezi tisa wakati baba ya mtoto wake wa nne alipomfukuza.

•Akothee ameeleza kuwa kufukuzwa kwake na mumewe huyo wa zamani kulifanya asitamani tena kuishi Ulaya.

Akothee na baby daddy wake mzungu
Image: HISANI

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kuwa alilazimika kurudi Kenya kutoka Uswizi baada ya mumewe kumfukuza takriban miaka kumi na minne iliyopita.

Mama huyo wa watoto watano amesema alikuwa na ujauzito wa miezi tisa wakati baba ya mtoto wake wa nne alipomfukuza.

Amesema mume huyo wake wa zamani alidai kuwa hakuwa tayari kuwa na mke ndiposa akamfukuza.

"'Rudi Afrika sina nguvu wala familia ya kutunza mwanamke mjamzito, siko tayari hata kuwa na mke' alisema baba mtoto wangu 👏💪," Akothee alisimulia kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 amekiri kuwa alipatwa na mawazo ya kujitoa uhai baada ya kupigwa teke na baby daddy huyo wake.

Nilifikiria kujitupa kwenye treni zinazopita, watoto wangu walikuwa wakinipigia simu mara kwa mara nchini Kenya, haswa Vesha, nilikaa kwenye baridi huko Basel BBB wakati wa msimu wa baridi mwezi Februari kwa usahihi 🙆‍♂️ mikahawa yote ilikuwa imefungwa na nilikuwa karibu kuachwa peke yangu, kwa wale wa Ulaya wanajua inavyojisikia kwenye vituo vya treni masaa ya usiku wakati treni zinafungwa," Alisimulia.

Akothee ameeleza kuwa kufukuzwa kwake na mumewe huyo wa zamani kulifanya asitamani tena kuishi Ulaya.

"Sitamani chochote, nakuja hapa kufanya mambo yangu na kurudi AFRICAAAAA," Alisema. 

Kwa kawaida, rais huyo wa single mothers wa kujitangaza huwa hazungumzi mengi kuhusu baba huyo wa mwanawe Prince Ojwan'g.

Wawili hao walikutana mwaka wa 2008 katika mkahawa mmoja ulioko eneo la Shanzu, kaunti ya Mombasa.

Akothee ameonekana kuwa na uhusiano mzuri na baby daddy wake wengine wawili zaidi ya baba Ojwang'.

Amekuwa akiwasherekea hadharani Jared Okello na Baba Oyoo mara kwa mara  kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwanamuziki huyo ana watoto watatu kutoka kwa ndoa yake ya kwanza na watoto wengine wawili ambao alipata na wazungu kutoka Uswizi na Ufaransa.