Akothee amweleza mwanawe kwa nini alichumbiana na babake mzungu licha ya umri wake mkubwa

"Umri ni nambari tu. Baba (Dominic) alikuwa na nguvu na alionekana mzuri sana," alisema.

Muhtasari

•Akothee alikabiliwa na maswali kuhusu jinsi alivyokutana na baba ya mtoto wake wa mwisho na kwa nini alichumbiana naye licha ya pengo kubwa kati ya umri wao.

•Akothee alilalamika kwamba mzazi huyo mwenzake alimlinda sana mwanao na hata angewakataza watu wengine kumgusa.

Papa Oyoo (Dominic) na Akothee
Papa Oyoo (Dominic) na Akothee
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumapili, mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee alikuwa na maelezo ya kuwafanyia watoto wake wawili wadogo wanaoishi Ufaransa, Prince Ojwang na Prince Oyoo.

Wawili hao walimkabili mama yao ambaye kwa sasa amewatembelea Ufaransa kwa maswali kuhusu jinsi alivyokutana na baba ya mtoto wake wa mwisho na kwa nini alichumbiana naye licha ya pengo kubwa kati ya umri wao.

Akothee alikutana na baby daddy wake wa tatu, Bw Dominic Decherf  mwongo mmoja uliopita wakachumbiana kwa muda kabla ya kutengana. Umri halisi wa Dominic haujulikani wazi  lakini ni dhahiri amemshinda sana Akothee kwa miaka.

"Umri ni nambari tu. Baba (Dominic) alikuwa na nguvu na alionekana mzuri sana. Alikuwa mrefu na mwenye upendo," mwanamuziki huyo aliwaelezea wanawe alipoulizwa kwa nini alimpenda licha ya umri wake mkubwa.

Bw Dominic alifichua kuwa mama huyo wa watoto watano ndiye aliyekutana naye.Akothee hata hivyo alibainisha wazi kuwa mzungu huyo anayeishi Ufaransa ndiye alimpenda kisha wakaanza mahusiano.

"Nilipokutana na baba (Dominic), Alfons alikuwa na umri wa mwezi mmoja tu, baba alinialika Djibouti. Nilikwenda na Alfons alinitendea kama malkia. Alininunulia tiketi ya eneo la biashara pamoja na mtoto, ilikuwa mara yangu ya kwanza katika eneo la biashara," Akothee alimwambia mwanawe Oyoo.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alidokeza kwamba mahusiano yao yalianza kusambaratika baada ya Bw Dominic kuelekeza mawazo yote kwa mtoto wao na kuonekana kuwasahau wengine.

Alilalamika kwamba mzazi huyo mwenzake alimlinda sana mwanao na hata angewakataza watu wengine kumgusa.

"Dominic alikuja na umakini wote kwa Dominic na watu wengine wote ndani ya nyumba haikuwa chochote kwake," alisema.

Akothee alikutana na Dominic miezi michache baada ya kutofautiana na baba mtoto wake wa pili ambaye alidai alimfukuza akiwa mjamzito.

Mara nyingi amekuwa wazi kuzungumzia uhusiano mzuri kati yake na mzazi huyo mwenzake wa mwisho anayeishi na wanawe wawili.