Akothee aonyesha zawadi maalum aliyopewa siku ya harusi yake, afichua bado hajazifungua

Akothee alifanya harusi ya kifahari mnamo Aprili 10, 2023 lakini ndoa hiyo ilidumu kwa takriban miezi miwili pekee.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alifichua kwamba bado hajafungua zawadi ambazo alipokea mnamo siku ya harusi yake na Denis Shweizer.

•“Asante kwa aliyenizawadi, asante kwa kuja kwenye harusi/siku yangu ya kuzaliwa hata kama mchezo iliisha mapema," Akothee alisema.

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Jumatatu, mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee alijitokeza akiwa amevalia rinda fupi nyekundu alikuwa akienda na Wakenya wengine katika zoezi la upandaji miti.

Mwimbaji huyo ambaye maisha yake yamezingirwa na drama nyingi alishiriki video fupi akiwa amevalia vazi hilo maridadi na kufichua kuwa ni miongoni mwa zawadi nyingi alizopokea mnamo siku ya harusi yake mapema mwaka huu.

Akothee alitumia nafasi hiyo kumshukuru aliyemzawadia nguo hiyo na kumtambua kwa kufika kwenye harusi yake licha ya jinsi mambo yalivyoisha.

“Rinda ndogo nyekundu ni miongoni mwa zawadi zangu za harusi/siku ya kuzaliwa. Bado sijafungua zawadi lakini sikuweza kushikilia zawadi hii,” Akothee alisema kwenye video hiyo aliyoshiriki kwenye mitandao ya kijamii.

Aliongeza, “Asante kwa aliyenizawadi, asante kwa kuja kwenye harusi/siku yangu ya kuzaliwa hata kama mchezo iliisha mapema, nguo imenitosha. Asante.”

Katika video hiyo, alionekana akimkumbatia mwanamume ambaye alishiriki mazungumzo fupi naye kabla ya wao kuandamana na kukutana naaliyekuwa mpenzi wake, Nelly Oaks.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mama huyo wa watoto watano kuthibitisha kuwa ndoa yake ya kipindi kifupi na mumewe mzungu, Denis ‘Omosh’ Schweizer tayari imevunjika.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alithibitisha kuvunjika kwa ndoa yake na Denis Shweizer mwisho mwa mwezi Oktoba. Alithibitisha hayo alipokuwa akishiriki kipindi cha moja kwa moja na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kipindi hicho, alithibitisha kwamba aligura ndoa yake ya muda mfupi mnamo mwezi Juni wakati yeye na Omosh walipokuwa kwenye fungate.

“Nimehama kutoka kwa mahusiano hayo. Hayapo tena. Ninataka kuwaaambia kwamba nilitoka kwenye uhusiano huo mwezi Juni. Hata hivyo sitaeleza kwa undani,” Akothee alisema.

Aliongeza, “Nilifurahia ndoa yangu, nilifurahia harusi yangu. Sijutii chochote. Nilifanya harusi yangu mnamo siku ya kuzaliwa kwangu ndio ikiwa tu mambo yangeenda vibaya, kama wamefanya, basi singekuwa na majuto yoyote.”

Akothee alisema aligura ndoa yake walipokuwa wakifurahia fungate yao baada ya kujifunza mambo kadhaa ambayo hakujua hapo awali.

Wakati huo, aliweka wazi kuwa yuko single akibainisha kwamba hakuna wakati hata ataruhusu mwanaume kumuathiri kisaikolojia.

“Mimi ni mtu ambaye silazimishi mambo. Wakati haifanyi kazi kwangu, hata ikiwa inakufanyia kazi, haifanyi kazi. Sababu ya kutodumu katika mahusiano yenye sumu ambayo sielewi ni kwa sababu pesa zangu ziko kichwani mwangu. Wakati ninapomruhusu mwanaume yeyote kunichafua kichwa, basi ananivuruga mfukoni,” alisema.