Aliyekuwa mpenzi wa Akothee kufunga ndoa hivi karibuni

"Siwezi kusubiri kusherehekea harusi yake, na ninamtakia kila la kheri," Akothee alisema.

Muhtasari

•Akothee aliwaambia mashabiki wake kwamba anafurahia maendeleo ya meneja huyo wake wa zamani aliyechumbiana naye kwa muda.

•Akothee alithibitisha kutengana kwake na Nelly Oaks takriban miezi mitano iliyopita

Nelly Oaks na Akothee
Nelly Oaks na Akothee
Image: INSTAGRAM//NELLY OAKS

Aliyekuwa mpenzi wa mwimbaji Akothee Nelly Oaks atafunga pingu za maisha na mpenzi wake hivi karibuni.

Ingawa hakuna habari za kutosha kuhusu harusi hiyo, Hivi majuzi Akothee aliwaambia mashabiki wake kwamba anafurahia maendeleo ya meneja huyo wake wa zamani aliyechumbiana naye kwa muda.

"Nelly anaendelea vizuri na ako na maisha yake, siwezi kusubiri kusherehekea harusi yake, na ninamtakia kila la kheri," alisema.

Mama huyo wa watoto watano aliendelea kumsifu Nelly Oaks, akimtaja kuwa mtu wa kipekee adimu kwa kubaki mtulivu baada ya wao kutengana.

"Nelly atabaki kuwa sehemu ya familia yangu, tuliachana kwa ajili ya ukuaji, sasa tumuombee apate mwanamke mwema aache kuishi maisha ya zamani," alisema.

"Msaidieni pale mnapoweza, kama sivyo, nyamaza. Nimeblock karibu wanawake 300 na wanaume 400 kuweka picha zake kwenye ukurasa wangu."

Akothee alithibitisha kutengana kwake na Nelly Oaks takriban miezi mitano iliyopita baada ya wao kukosa kuonekana pamoja kwa muda.

Alisema kuachana na Nelly Oaks ilikuwa ni uamuzi wa kibinafsi tu na alihitaji wakati wa kuzingatia furaha yake mpya bila usumbufu mdogo.

Mama huyo wa watoto watano aliongeza kuwa ni uamuzi kwa mtu yeyote kumwacha yeyote wakati wowote anaotaka.

Kwa sasa Akothee yupo kwenye mahusiano na mzungu kijana ambaye amepatia jina Bw Omondi.