"Ananitia woga!" Mbosso hatimaye ajibu kuhusu Mkenya anayefanana naye aliyedai DNA

Mbosso alidai kwa kuzingatia umri wake, kuna uwezekano Mkenya huyo anaweza kuwa babake.

Muhtasari

•Demah B alidai kuwa msanii huyo wa WCB ni baba yake na hata akadai kipimo cha DNA kifanyike ili kuthibitisha hilo.

•Wakati akiwahutubia wanahabari , Mbosso hata hivyo alipuuzilia mbali uwezekano wa kuwa baba ya msanii huy chipukizi.

Mbosso na Demmah B
Mbosso na Demmah B
Image: Facebook

Staa wa muziki Bongo, Mbwana Yusuf Kilungi amekanusha madai kuwa yeye ndiye baba mzazi wa msanii chipukizi wa Kenya anayefahamika kwa jina la Demah B.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na waandishi wa habari mbalimbali, Demah B alidai kuwa msanii huyo wa WCB ni baba yake na hata akadai kipimo cha DNA kifanyike ili kuthibitisha hilo.

Msanii huyo alisema kwamba Mbosso ni baba yake aliyemtelekeza na akadai sasa anateseka huku staa huyo wa bongo akiendelea kupunja mazuri maisha nchini Tanzania.

“Amekataa kabisa, huyo jamaa [Mbosso] tuseme tu ni kama amekataa majukumu, anaogopa DNA. Kwangu mimi niko tayari kufanya DNA tujue kama mimi ni mtoto wake, sababu ameniacha nateseka hapa Kenya na babangu yuko kule majuu na ishajua ni yeye, hiyo kitu inaniuma sana,” Demah B alisema.

Aliendelea, “Yeye yuko tu naona anapost na anajua tu yuko na mtoto hapa Kenya, mtu anakuja tu amepata umetulia anakuapiza kijana unateseka na babaki yuko majuu, inaniumiza sana. Mimi nataka kumuambia Mbosso, chenye nataka kujua ni ukweli tu, tukuje tufanye DNA tujue ukweli uko wapi. Haiwezekani kwamba mimi nateseka pahali nje na yeye yuko pale juu yuafaidika na kupata kila kitu na mtoto wake hapa. Yeye yuaona kila kitu macho, pua, maskio na vitendo vyote ni vyake,”

Wakati akiwahutubia wanahabari wa Kenya mjini Mombasa, Mbosso hata hivyo alipuuzilia mbali uwezekano wa kuwa baba ya msanii huy chipukizi.

Mbosso alisema kuwa Demah B anaonekana kuwa mkubwa kwa umri kuwa mwanawe na kudai kuwa badala yake, Mkenya huyo anaweza kuwa babake.

“Yule mtoto wangu, yule namuona kupitia mitandao ya kijamii. Tatizo yeye sio mtoto. Kutokana na umri wake, kutokana na jinsi yeye mwenyewe alivyo, ananitia uoga hadi mimi mwenyewe nahisi yeye ndiye babangu. Yeye anaonekana mkubwa hadi kanizidia mimi. Kwa hiyo yeye kama anaona mimi ni baba yake, pia mimi nahisi yeye ndiye babangu. Sijui itakuwaje hapo,” Mbosso alisema.