"Anaumia sana, hana chochote!" Mkewe Stivo afunguka kuhusu matatizo ya kifedha ya msanii huyo

Grace alimshtumu meneja wa Stivo kwa kumhujumu na kujinufaisha na jasho lake.

Muhtasari

•Grace alibainisha kuwa licha ya kuwa na jina kubwa, mumewe anakabiliwa na changamoto za kifedha kwani havuni chochote kutokana na muziki wake.

•Alibainisha kwamba matatizo ya kifedha nyumbani hufanya wanagombana mara kwa mara ila wanavumilia tu.

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Mke wa Stivo Simple Boy, Grace Atieno amefunguka kuhusu masaibu ambayo yeye na msanii huyo wanapitia nyumbani.

Katika mahojiano na Vincent Mboya, mrembo huyo kutoka Taita Taveta alibainisha kuwa licha ya kuwa na jina kubwa, mumewe anakabiliwa na changamoto za kifedha kwani havuni chochote kutokana na muziki wake.

Grace alimshtumu meneja wa Stivo kwa kumhujumu na kujinufaisha na jasho lake.

“Stivo anapitia maisha magumu. Yeye ni mtu muoga na kijana mpole. Kuna mambo anapitia lakini ni muoga wa kuongea. Kuna marafiki wake na mashabiki hutamani kuchat na yeye lakini hawawezi kumkuta,” Grace alilalamika.

Aliongeza, “Najua watu wengi wanajua Stivo ni yeye hutumia Tiktok yake na Instagram, lakini sio yeye. Wengi huwa wanalalamika kwamba wanataka kumsaidia na kitu kidogo lakini hawamkuti. Yaani anapitia changamoto nyingi tu.. Hana akaunti yoyote anayotumia. Meneja wake ako na kila kitu chake. Hata kumpata, huwezi kumkuta kwa urahisi.”

Bi Grace alifichua kwamba mumewe ata hafahamu  kiasi cha pesa ambacho huwa analipwa kwa kila shoo. Alisema meneja wake ndiye anayendeleza na kusimamia kila kitu ikiwemo akaunti zote za mitandao ya kijamii, mawasiliano na hata malipo.

Alibainisha kwamba matatizo ya kifedha nyumbani hufanya wanagombana mara kwa mara ila wanavumilia tu.

 “Tunapitia magumu ni ile tu huwezi kutoka nje kuomba mtu nini na nini, tunavumilia tu. Wakati mwingine tunagombana kutokana na hizo tu changamoto lakini ukimwambia aende aongee na meneja wake mambo ya hela ajisimamie mwenyewe anaogopa,” Grace alisema.

“Kuna saa zingine twapata, saa zingine tunakosa. Yeye hana kazi eti anaweza akasema atatoka huku nje afanye ili apate pesa atafute chakula. Ni hiyo tu kazi moja ambayo anategemea na hiyo kazi ambayo anategemea hamna chochote. Meneja wake ndiye amebeba pesa, amebeba kila kitu,” alilalamika.

Grace sasa ameomba watu walio na nia ya kumsaidia mtunzi huyo wa kibao ‘Mihadarati’ kumfikia moja kwa moja badala ya kumtumia meneja huyo.

“Akaunti zake, hakuna yenye anasaidika nayo. Anaumia sana. Stivo hana chochote Wakenya huku nje wanajua Stivo anaishi maisha mazuri lakini sio maisha mazuri ambayo anaishi. Meneja wake ni mtu ambaye anamkulia sana. Stivo ni mtu ambaye ananyanyasika sana na mimi sijapenda. Hakuna kitu anatumia, yeye yuko tu kwa hivyo ata ni vigumu kupata naye,” alisema.

Grace aliwaomba Wakenya ambao wangependa kuwasiliana na Stivo ama  kumsaidia kumfikia kupitia  namba yake 0759 325 783.