Azziad azungumzia kupata kazi serikalini kwa kuhusika kimapenzi na waziri Ababu Namwamba

Azziad alikanusha madai kwamba alitumia mwili wake kupata uteuzi mkubwa wa serikali.

Muhtasari

•Azziad alikanusha madai kwamba alipewa kazi kubwa ya serikali miezi kadhaa iliyopita kwa kupendelewa na waziri Namwamba.

•Azziad alifichua kuwa hajali sana kwani watu ambao ni muhimu kwake wakiwemo wazazi na mpenzi wake wanamuunga mkono.

Azziad Nasenya na Ababu Namwamba
Image: HISANI

Mtayarishaji maudhui na mwanahabari mashuhuri wa Kenya Azziad Nasenya amefunguka kuhusu kuhusishwa kimapenzi na waziri Ababu Namwamba mapema mwaka huu.

Katika mahojiano na Mungai Eve, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 alikanusha madai kwamba alipewa kazi kubwa ya serikali miezi kadhaa iliyopita kwa kupendelewa na waziri huyo wa Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa.

Azziad aliweka wazi kuwa alipewa kazi hiyo kwa sababu ana sifa zilizohitajika na kubainisha haina uhusiano wowote na yeye kudaiwa kuwa kwenye mahusiano na waziri Namwamba.

"Nadhani inasikitisha. Ukiangalia pia mimi nimeenda shule, niko na akili. Singekuwa hapa kama akili na kama sina timu nzuri nyuma yangu,” Azziad said.

Mtumbuizaji huyo wa tiktok alishangaa ni kwa nini Wakenya waliamua kumshambulia baada ya kuteuliwa katika kazi ya serikali ilhali kamati nzima ya Talanta Hela iliyochaguliwa ilikuwa na wanawake wengine.

Hata hivyo, alisema huenda watu waliamua kumshambulia kwa sababu yeye ni mdogo na wanaona hawezi kufikia mafanikio yote aliyoweza kujizolea tayari, jambo ambalo alijitetea akisema;

“Nimeenda shule, nimemaliza. Mimi ni mwanafunzi katika Taasisi ya Mawasiliano ya Umma ya Kenya. Mimi kitaaluma ni mwanahabari na ndiyo maana ninafanya kazi katika redio. Unamaanisha nini kwamba sistahili? Unamaanisha nini?,” alisema.

Azziad alikanusha madai kwamba alitumia mwili wake kupata uteuzi huo wa kifahari na kutoa changamoto kwa wale wanaohisi ni hivyo pia kufanya vivyo hivyo. Wakati huo huo, alibaini kuwa kamati ya Talanta Hela ilikuwa timu yenye usawa kwani kila mtu anawakilisha kikundi fulani cha watu, yeye akiwakilisha vijana.

Mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 23 pia alikiri kwamba shutuma kama hizo humfanya ajisikie vibaya kwa sababu kama binadamu mwingine yeyote, pia yeye ana hisia.

Hata hivyo alifichua kuwa hajali sana kwani watu ambao ni muhimu kwake wakiwemo wazazi na mpenzi wake wanamuunga mkono.

“Nina mpenzi wa kunisapoti ambaye namshukuru, nina wazazi wanaoniunga mkono. Inahisi vibaya kwa sababu mwisho wa siku mimi ni binadamu. Lakini tena, wacha turudi kwa watu ambao ni muhimu, hawajali. Hawawaamini watu hao. Watu wa maana huwa wananipigia simu kujua kama niko sawa. Nina mfumo wa usaidizi nyuma ya mtandao ambao hupiga simu kila wakati haya yote yanapotokea," alisema.