Mridhi wa Keroche Anerlisa Muigai hatimaye amevunja kimya baada ya aliyekuwa mke wake Ben Pol kudai kwamba hakufurahia ndoa yao.
Ben akiwa kwenye mahojiano na mtangazaji wa Tanzania Millard Ayo, alisema kwamba ndoa yao ya miaka mitatu ilihusu sana kujionyesha kwenye mitandao ya kijamii badala ya kufurahia manufaa halisi ya ndoa.
"Kusema kweli nisiwe muongo, ukitoa picha za Instagram na nini, sijaenjoy sana ndoa. Ile mipango ya ndoa, tutengeneze watoto tuzae na nini, sijawahi kuona. Sikuona ndoa kama ninavyoona na watu wengine," alisema.
Katika majibu yake baada ya mahojiano hayo kupakiwa mitandaoni, Bi Anerlisa alimkosoa staa huyo wa Bongo na kumshtumu kwa kuzungumza mambo ambayo ni tofauti na uhalisia uliopo nyuma ya pazia.
Mjasiriamali huyo pia alimshutumu mwimbaji huyo kwa kujinufaisha na ukimya wake kuhusu masuala ya ndoa yao iliyovunjika.
"Ben naona umenizoea, na umechukua ukimya wangu kuwa na udhaifu.. umekuwa na haki ya kumwambia anayekuhoji asiulize kunihusu," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
"Kwa nini kila wakati unanifanya nionekane mbaya, lakini kwa siri, unanitumia ujumbe tofauti na unavyozungumza," aliuliza.
Binti huyo wa seneta wa Nakuru Tabitha Karanja zaidi aliendelea kumthubutu Ben kuonyesha screenshots za jumbe ambazo amekuwa akimtumia kwenye simu kati ya siku ya Krismasi na Januari 4.
"Nina mengi ya kusema au kuonyesha kukuhusu, lakini nachagua kuwa mwanamke,"
Anerlisa sasa amemtaka mwimbaji huyo wa Bongo RnB kukoma kabisa kuzungumza kumhusu katika jukwaa lolote..
Wakati wa mahojiano, Ben alidokeza kuwa anahisi huenda alitumiwa na mke huyo wake wa zamani kutimiza malengo yake maishani.
"Naona kama niliingia kwenye picha ili kuleta ule ukamilifu!" alisema.
Mwimbaji huyo alibainisha kwamba uhusiano wake na Anerlisa ulikuwa wa kwanza kabisa wa kweli kuwahi kutokea katika maisha yake na hivyo alikuwa na matumaini makubwa ya ndoa nzuri naye.
Alikiri kuwa alikuwa amewekeza hisia na mapenzi yake yote kwa kipusa huyo kabla ya mambo kuenda mrama.
"Kiwango cha upendo, kiwango cha kujitolea na kiwango cha kujitoa ambacho nilikuwa nimetoa kwake haijawahi kutokea hapo awali. Sijahi kumpenda mtu mwingine kabla yake. Yalikuwa mahusiano ya kwanza kuzama kabisa na nilikuwa sawa," alisema.
Ben Pol aliweka wazi kwamba ndoa yao haikuvunjika kwa sababu ya masuala ya ukosefu wa uaminifu kwa kila mmoja.
Licha ya kutengana kwao takriban miaka miwili iliyotokea na yote yaliyotokea baina yao, hana kinyongo chochote dhidi yake. Pia alidokeza kwamba bado ana hisia za mapenzi kwa Anerlisa ndani ya moyo wake.
"Tunazungumza.Tulichat kwenye WhatsApp mwezi Juni. Kulikuwa na vitu vyake huku, nilikuwa naenda Nairobi, nikawa naenda kumpatia. Lakini sikuendea mwenyewe, nilimwagiza mtu ampelekee lakini tulikuwa tunazungumza tu," alisema.
Aidha, Ben Pol alibainisha kuwa ingawa ndoa yao haikufanikiwa, mke huyo wake wa zamani ana haki ya kupendwa na mwingine.