Bill Nass akiri ukweli kuhusu uhusiano wake na Hamisa Mobetto baada ya kuhusishwa na mtoto wake

Rapa huyo alifichua kuwa alifahamiana na Hamisa wakati wote wawili walikuwa wamejipata kwenye matatizo sawa.

Muhtasari

•Bill Nass amekana kuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi Hamisa na kuweka wazi kuwa uhusiano wao ni wa kirafiki tu.

•Rapa huyo pia alijitenga mbali na madai yanayomhusisha na mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo, Dylan Abdul Naseeb.

Bill Nass, Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM

Rapa wa mashuhuri wa Tanzania William Nicholaus Lyimo almaarufu Bill Nass ameweka mambo wazi kuhusu uhusiano wake halisi na mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Katika mahojiano na Wasafi Media, mume huyo wa Nandy alipuuzilia mbali tetesi za kuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mlimbwende huyo na kuweka wazi kuwa uhusiano wao ni wa kirafiki tu.

Alifichua kuwa alifahamiana na Hamisa wakati wote wawili walikuwa wamejipata kwenye matatizo sawa na polisi na baada ya kujuana, wakawa marafiki wakubwa lakini kwa mujibu wake, hawakuwahi kuhusiana kimapenzi.

“Mimi sijawahi kuwa na mahusiano na Hamisa. Ilitokea kuna wakati tulikuwa na urafiki sana, tukawa tunacommentiana, tunashauriana kuhusu baadhi ya vitu, tulikuwa na urafiki. Hakukuwa na jambo mbaya lolote kwa sababu ni urafiki ambao ninamfahamu, ananifahamu, ilitokea. Tulikutana kwenye matatizo unakumbuka wakati nimepata skendo yangu ya video, na wao walikuwa na kesi yao ya video kwa hiyo tukatokea kuwa marafiki kwa sababu tulikutana na polisi na walikuwa wanatutisha,” Bill Nass alisimulia.

Aliongeza, “Ikawa urafiki, baadaye tulikutana katika maisha mengine. Hakukuwa na la ziada zaidi ya hilo.  Ikaja hizo stori. Zilipoanza ata huyo mhusika mwenyewe hakupenda kwa sababu alishangaa mbona kukawa na stori kama hizo. Mimi naheshimu kwa sababu nimekuwa na marafiki wa kike nikiwa shule na nikiwa wapi, najua ni namna gani naweza kumtia doa. Sasa imefika level ya mtoto. Mtoto ni kiumbe na ana baba yake na ni propaganda.”

Mwimbaji huyo wa kibao 'Puuh' pia alijitenga mbali na madai yanayomhusisha na mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo, Dylan Abdul Naseeb.

Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakihusisha mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo na Bill Nass na hata kuibua madai kuwa wanafanana sana. Bill Nass hata hivyo amedokeza kuwa tetesi za yeye kuwa baba wa mtoto huyo ni propaganda tu na kusema kuwa tayari Hamisa alikuwa na watoto wake wawili wakati walipofahamiana.

“Ni propaganda za watu. Sijui nia au dhumuni ya hiyo habari ilianzia wapi lakini mimi mtoto hanihusu kwa namna moja au nyingine. Wakati ambao tulifahamiana, tayari alikuwa na watoto wake wawili. Kwa mara ya kwanza namuona alikuwa na watoto. Kutokea hapo sijawahi kuwa na issue yoyote,” Bill Nass alisema.

Aidha, alisisitiza kwamba yeye anafahamu fika kuwa baba ya mwanawe Hamisa Mobetto ni bosi wa WCB Diamond Platnumz.