Rapa wa Tanzania William Nicholaus Lyimo almaarufu Bill Nass amejitenga na mtoto wa mwanamitindo Hamisa Mobetto, Dylan Abdul Naseeb.
Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakihusisha mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo na Bill Nass na hata kuibua madai kuwa wanafanana sana.
Katika mahojiano na Wasafi Media, mwimbaji huyo aliyevuma kwa jina la ‘puuh’ alidokeza kuwa tetesi za yeye kuwa baba wa mtoto huyo ni propaganda tu na kusema kuwa tayari Hamisa alikuwa na watoto wake wawili wakati walipofahamiana.
“Ni propaganda za watu. Sijui nia au dhumuni ya hiyo habari ilianzia wapi lakini mimi mtoto hanihusu kwa namna moja au nyingine. Wakati ambao tulifahamiana, tayari alikuwa na watoto wake wawili. Kwa mara ya kwanza namuona alikuwa na watoto. Kutokea hapo sijawahi kuwa na issue yoyote,” Bill Nass alisema.
Mume huyo wa malkia wa bongofleva Nandy aliweka wazi kuwa hajawahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Hamisa Mobetto.
Alibainisha kuwa uhusiano wake na mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz ni urafiki tu na hakuna zaidi ya hilo.
“Huyu mtoto hanihusu kwa namna yoyote kwa sababu sijawahi kuwa na mahusiano na mama yake zaidi ya urafiki. Ndio maana huwa haleti shida kwa mke wangu,” alisema.
Billnass alifichua kuwa alifahamiana na Hamisa wakati wote wawili walikuwa wamejipata kwenye matatizo karibu sawa na polisi.
Ilikuwa ni baada ya kujuana ndipo wakawa marafiki wakubwa lakini kwa mujibu wa rapa huyo, hawakuwahi kuhusishwa kimapenzi.
“Mimi sijawahi kuwa na mahusiano na Hamisa. Ilitokea kuna wakati tulikuwa na urafiki sana, tukawa tunacommentiana, tunashauriana kuhusu baadhi ya vitu, tulikuwa na urafiki. Hakukuwa na jambo mbaya lolote kwa sababu ni urafiki ambao ninamfahamu, ananifahamu, ilitokea. Tulikutana kwenye matatizo unakumbuka wakati nimepata skendo yangu ya video, na wao walikuwa na kesi yao ya video kwa hiyo tukatokea kuwa marafiki kwa sababu tulikutana na polisi na walikuwa wanatutisha,” alisimulia.
Aliongeza, “Ikawa urafiki, baadaye tulikutana katika maisha mengine. Hakukuwa na la ziada zaidi ya hilo. Ikaja hizo stori. Zilipoanza ata huyo mhusika mwenyewe hakupenda kwa sababu alishangaa mbona kukawa na stori kama hizo. Mimi naheshimu kwa sababu nimekuwa na marafiki wa kike nikiwa shule na nikiwa wapi, najua ni namna gani naweza kumtia doa. Sasa imefika level ya mtoto. Mtoto ni kiumbe na ana baba yake na ni propaganda.”
Bill Nass alisisitiza kwamba anafahamu baba ya mwanawe Hamisa Mobetto kuwa bosi wa WCB Diamond Platnumz.
Aidha, aliweka wazi kwamba ana uhusiano mzuri na mwimbaji huyo mwenzake na kubainisha kwamba hajawahi kubishana naye kuhusu suala la mtoto huyo.
“Mimi naamini baba ya mtoto ni Diamond. Diamond ni kaka ambaye tuna uhusiano mzuri. Ramadhan mwaka huu nilifuturu kwake.Tuliongea tunapiga stori. Kama kungekuwa na dhamira yoyote mbaya au kitu chochote, ni vitu vingine unaweza kumwambia mtu, kiukweli mimi ni mtu ambaye angeweza kunitoka moyoni,” alisema.
Kwa muda mrefu, kumekuwa na mjadala kuhusu baba halisi wa mtoto wa Hamisa Mobetto huku Diamond ambaye anaaminika kuwa mhusika akionekana kujitenga naye na kutojivunia yeye kama anavyofanya na watoto wake wengine.