Daddy Owen afichua kwa nini hakuvua pete baada ya talaka na aliyekuwa mkewe

"Nilikaa nayo nikasema nitatoa siku nataka kutoa. Ilifika mahali nikaambia wasee mwenyewe najua siku nataka kutoa," Owen alisema.

Muhtasari

•Daddy Owen alibainisha kuwa alikaa na pete hiyo kwa muda mrefu kama njia ya kuonyesha upinzani kwa watu waliokuwa wakimshinikiza kuitoa

•Daddy Owen alidokeza kwamba alitaka kudhibiti simulizi yake mwenyewe kwani ilifikia hatua ambapo kila mtu alitaka kumshauri nini cha kufanya.

Daddy Owen na aliyekuwa mkewe Farida Wambui
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amefunguka kwa nini alichukua muda kabla ya kuvua pete yake ya ndoa baada ya talaka na aliyekuwa mkewe, Farida Wambui.

Akizungumza katika mahojiano na Mwafrika kwenye kipindi cha Iko Nini Podcast, Owen alibainisha kuwa alikaa na pete hiyo kwa muda mrefu kama njia ya kuonyesha upinzani kwa watu waliokuwa wakimshinikiza kuitoa.

“Nilikaa nayo zaidi ili kuwa mkaidi zaidi. Kwa wakati mwingine watu walikuwa wakisema “toa hiyo pete”, “tupa hiyo pete” ila mimi nilikuwa nasema sio kubwa lakini sio vile wasee walikuwa wanasema ni kama siamini, ni kama nataka kurudi,” Daddy Owen alisema.

Aliongeza, “Kwangu nilikaa tu nayo nikasema nitatoa siku nataka kutoa. Ilifika mahali nikaambia wasee mimi mwenyewe najua siku nataka kutoa.

Daddy Owen alidokeza kwamba alitaka kudhibiti simulizi yake mwenyewe kwani ilifikia hatua ambapo kila mtu alitaka kumshauri nini cha kufanya.

“Ilifika mahali hata majibu nilikuwa napatia wasee kulingana na vile nataka. Ilifika mahali nataka kudhibiti simulizi yangu mwenyewe, chochote nilikuwa naambia watu sio nilichotaka kwa kweli. Ilifka mahali ni kama nilikuwa nadhibitiwa na yaliyokuwa yakiendelea karibu nami.”

"Sikutaka kupoteza mimi ni nani. Nadhani mwanamume lazima uwe mkaidi kwa njia fulani. Kwa kuwa mkaidi, hukupa ubinafsi na kukuonyesha wewe ni nani kama vile ulivyo kama mwanaume. Bado naweza kusema HAPANA na inabaki kuwa HAPANA.”

Katika mazungumzo hayo, mwanamuziki huyo aliweka wazi kwamba alikuwa kwenye ndoa na mzazi huyo mwenzake huyo kwa takriban miaka mitano kabla ya kuvunjika kwa njia mbaya.

Daddy Owen alibainisha kuwa hadithi nyingi zilitokea baada ya talaka, ambazo baadhi anasema zilikuwa za kweli ilhali zingine zilikuwa habari za uwongo.

“Ndoa yangu kuisha iliisha. Haikuisha vizuri. Kwa kweli, kuna stori nyingi zilitoka. Zingine kweli, zingine hazikuwa kweli lakini ndoa yangu iliisha. Ilichukua muda kujua nini cha kufanya baadae. Haikusha poa, kwa kweli mlisikia stori mob,” Daddy Owen alisema.

Mwimbaji huyo na Bi Faridah Wambui walikutana mwaka wa 2012, wakafunga ndoa mwaka wa 2016 kabla ya kuachana 2020.