Daddy Owen afunguka ukweli kuhusu uhusiano na Charlene Ruto

Daddy Owen na Charlene Ruto wameonekana wakishiriki muda pamoja mara kadhaa katika siku za hivi majuzi.

Muhtasari

•Daddy Owen amefunguka kuhusu uhusiano wake na Charlene Ruto, siku chache tu baada ya kuonekana wakishiriki muda mzuri pamoja.

•"Mbali na sisi kuwa marafiki tu, tunafanya kazi pamoja. Kuna miradi mingi tunafanya pamoja,” Daddy Owen alisema.

Image: INSTAGRAM// DADDY OWEN

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amefunguka kuhusu uhusiano wake na binti ya rais William Ruto, Charlene Ruto, siku chache tu baada ya kuonekana wakishiriki muda mzuri pamoja.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Daddy Owen ambaye alisikika kushtuka sana kwa kuhusishwa kimapenzi na binti ya rais aliweka wazi kuwa yeye ni rafiki mzuri tu kwake.

Pia alifichua kuwa yeye na Charlene Ruto wamekuwa wakifanya kazi pamoja katika miradi kadhaa ambayo hakufichua.

"Ni kazi tu, sisi tunapiga tu kazi!" Daddy Owen alisema.

Kuhusu kuonekana pamoja na Bi Charlene, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alieleza kuwa yeye na mrembo huyo kijana wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali pamoja.

"Mbali na sisi kuwa marafiki tu, tunafanya kazi pamoja. Kuna miradi mingi tunafanya pamoja,” alisema.

Aidha, Daddy Owen alidokeza kuwa sio kila mwanamke ambaye anaonekana naye ni mpenzi wake. Pia alisema kuwa hajui hali ya mahusiano ya bintiye rais licha ya wao kuwa marafiki.

Takriban miezi minne iliyopita, mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa hana haraka ya kutafuta mke mwingine baada ya kutengana na wa kwanza, Bi Faridah Wambui.

Katika mahojiano ya kipekee na Radio Jambo, Daddy Owen alisema kuwa katika kampeni yake ya kujaribu bahati katika kupata mrembo wa kijijini wa kuoa mapema mwaka huu, hakufanikiwa licha ya kuchukua muda mrefu kutafuta mmoja.

Owen alisema kuwa hata hivyo, pia alishikika sana na kazi nyingi kiasi kwamba alipoteza azma ya kumpata mmoja.

“Mimi sikufanikiwa, kazi imekuwa nyingi. Sasa hivi, kazi imekuwa nyingi hata sina mpango wa kutafuta tena,” Daddy Owen alijibu.

Daddy Owen na aliyekuwa mke wake, Faridah Wambui walikutana mwaka wa 2012, wakafunga ndoa mwaka wa 2016 kabla ya kuachana 2020.