Diamond amtenga mtoto wake na Hamisa Mobetto huku akiwaleta pamoja wanawe wengine

Siku ya Ijumaa, Diamond alionyesha video nzuri ya watoto wake watatu wakicheza pamoja

Muhtasari

•Diamond alionekana pamoja na watoto wake watatu na mama yake Mama Dangote wakielekea uwanja wa ndege kwa gari lake la kifahari.

•Watoto wote watatu; Tiffah, Nillan na Naseeb Jr walionekana kushangazwa na kuvutiwa na uzuri wa ndege hiyo ya baba yao.

wakicheza pamoja
Prince Nillan, Tiffah Dangote na Naseeb Jr wakicheza pamoja
Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo, Naseeb Abdul Juma anaendelea kufurahia muda na watoto wake watatu, Tiffah Dangote, Prince Nillan na Naseeb Juniorr wikendi hii.

Watoto wawili wakubwa wa mwimbaji huyo, Tiffah na Nillan, ambao alizaa na mwanasosholaiti wa Uganda Zari Hassan wanaaminika kurudi naye nchini Tanzania kutoka Afrika Kusini wanakoishi na mama yao siku ya Alhamisi.

Naseeb Jr, ambaye ni mtoto wa staa huyo na mrembo wa Kenya, Tanasha Donna, ameonekana naye nchini Tanzania mara nyingi katika wiki kadhaa zilizopita na hata alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya nne katika nchi hiyo jirani upande wa kusini mapema mwezi huu.

Siku ya Ijumaa, Diamond Platnumz alionyesha video nzuri ya watoto wake watatu wakicheza pamoja. Pia alipakia video zaidi zake, watoto wake watatu na mama yake Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote wakielekea uwanja wa ndege kwa gari lake la kifahari.

Msafara wa magari mengine ya kifahari yaliwasindikiza walipokuwa wakienda kupanda ndege yake binafsi kuwapeleka Kigali, Rwanda kwa ajili ya Tuzo na Tamasha la Trace.

“Kigali, Rwanda one time for the @traceawardsfestival,” Diamond aliandika chini ya video yake akiwa na watoto wake ndani ya ndege ambayo alipakia Instagram.

Ndege hiyo, kama inavyoonekana kwenye video, ilikuwa imefanyiwa mapambo maalum kwa ajili ya mwimbaji huyo wa bongo fleva ikiwa na mito na viti viliandikwa jina lake na kubandikwa picha zake.

Watoto wote watatu; Tiffah, Nillan na Naseeb Jr walionekana kushangazwa na kuvutiwa na uzuri wa ndege hiyo ya baba yao.

“Ooh Mungu wangu, unaona ninachokiona, unaona ninachokiona sasa hivi? Ni Diamond Platnumz!!" Prince Nillan alieleza kwa mshtuko mara baada ya kuingia ndani ya ndege hiyo.

Nillan na Tiffah walisikika wakimuuliza baba yao ikiwa wanaweza kutumia ndege yake ya kibinafsi wakati wowote, siku yoyote wanayotaka.

"Ndiyo, kama mnavyotaka," Diamond alijibu.

Muungano wa Diamond na watoto wake watatu ulionekana kuwa wakati mzuri na wote walionekana kufurahia sana

Anayedaiwa kuwa mwanawe na mwanamitindo wa Tanzania Hamisa Mobetto hata hivyo hakuonekana pamoja nao. Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyo kuonekana kujitenga na mvulana huyo wa miaka 6. Huko nyuma amewahi kumkana waziwazi.