Diamond hatimaye amaliza ugomvi na Alikiba, amvulia kofia

Diamond alionyesha upendo mkubwa kwa Alikiba siku ya Jumapili.

Muhtasari

•Siku ya Jumapili, bosi huyo wa WCB kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka wazi wimbo wa Alikiba anaoupenda zaidi.

• Diamond alikiri kuwa baada ya kuwaza kwa kina aligundua kwamba yeye na Alikiba wanatofautiana katika mambo madogo madogo kama mashabiki na umaarufu.

Diamond Platnumz, Al8ikiba
Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongofleva Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amedokeza kwamba hali sasa ni shwari kabisa kati yake na mwimbaji mwenzake anayedaiwa kuwa hasidi wake wa muda mrefu, Alikiba.

Siku ya Jumapili, bosi huyo wa WCB kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka wazi wimbo wa Alikiba anaoupenda zaidi.

Diamond alikiri mapenzi yake makubwa kwa wimbo 'Asali' ambao mwenzake huyo aliutoa mwezi Septemba mwaka jana.

"Favourite 🏆🤍" (Wimbo pendwa) Diamond aliandika chini ya picha ya bango la wimbo huo wa Alikiba. 

Wengi wamechukulia hatua hiyo kama ishara kuwa Diamond hana kinyongo dhidi ya mwimbaji huyo mwenzake.

Wanamuziki hao wawili wakongwe wa Bongo wamekuwa wakidaiwa kuzozana kwa muda mrefu na mara kadhaa wamekuwa wakionyesha wazi ugomvi wao. Hata hivyo, wamezungumzia tofauti zao mara nadra tu

Katika wimbo wake wa ‘Nawaza’ alioutoa mapema mwaka jana, Diamond alikiri kuwa baada ya kuwaza kwa kina aligundua kwamba yeye na Alikiba wanatofautiana katika mambo madogo madogo kama mashabiki na umaarufu.

“Nilowaza leo nishawaza sana, mimi na Kiba ugomvi nikagundua ni ushamba na ujana wa kugombania mashabiki,” aliimba

Bosi huyo wa WCB alibainisha zaidi kuwa amekua katika tasnia ya muziki na hajishughulishi tena na masuala kama hayo.

Mwezi Machi mwaka jana, Diamond alisema kwamba yuko tayari kufanya kazi na Ali Kiba, endapo fursa itajitokeza.

Akizungumza kwenye mahojiano na Wasafi,  alisema usimamizi wake umejaribu kuwasiliana na Kiba ili wafanye kazi pamoja.

Nishapigia simu Menejimenti yake tukitaka tuandae show, nilishamwalika kwenye show zangu kabla hata ya Wasafi Festival, mimi sina noma yaani fresh tu," alisema.

Wakati huohuo, Diamond aliwashauri wasanii wenzake kukoma kuunda migogoro midogo kati yao ili kutafuta umuhimu.