Diamond Platnumz atuhumiwa kujigamba na saa feki ya mamilioni

Mwimbaji huyo amedaiwa kuwa na saa bandia aina ya 'Patek Philippe Nautilus 5711/1A.'

Muhtasari

•Imedaiwa kwamba saa ya Diamond ni tofauti kabisa kimuonekano kuanzia kwa umbo la kesi cha saa, fremu, saizi pamoja na tofauti zingine.

•Mtu anaweza kupata saa halisi ya Patek Philippe Nautilus akiwa na takriban Ksh 23.5 milioni au shilingi millioni 444 za kitanzania.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo, Diamond Platnumz amekosolewa baada ya kudaiwa kuwa na saa  bandia aina ya 'Patek Philippe Nautilus 5711/1A.'

Kulingana na akaunti ya @fakewatchbuster kwenye Instagram ambayo huripoti saa bandia, saa ya ambayo Diamond alionekana nayo katika mojawapo ya posti zake inayodaiwa kuwa Patek Philippe Nautilus 5711/1A yenye thamani ya mamilioni ya pesa si halisi.

Akaunti hiyo imedai kwamba saa ya Diamond ni tofauti kabisa kimuonekano kuanzia kwa umbo la kesi cha saa, fremu, saizi pamoja na tofauti zingine.

"@diamondplatnumz, kwa maoni yetu huyo ni Patek Philippe Nautilus 5711/1A bandia," @fakewatchbuster walisema kwenye Instagram.

Wapelelezi hao wa mitandaoni waliendelea  kutaja angalau tofauti saba kati ya saa ya Diamond na Philippe Nautilus 5711/1A halisi.

"Philippe Nautilus Carbon ya DiW halisi ina thamani ya takriban USD 190,000 kuenda juu,"  walisema @fakewatchbuster.

Mtu anaweza kupata saa halisi ya Patek Philippe Nautilus akiwa na takriban Ksh 23.5 milioni au shilingi millioni 444 za kitanzania.

Bila shaka, Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii mashuhuri na tajiri zaidi sio to Afrika Mashariki bali pia kote bara Afrika.

Hata hivyo, bosi huyo wa WCB amewahi kumulikwa na kukosolewa mara kadhaa kwa kuishi maisha bandia na kumiliki bidhaa ghushi.

Hapo awali, aliwahi kupuuzilia madai ya kuishi maisha feki na kudai kwamba yeye ana utajiri mkubwa sana kiwango ambacho hawezi akakivalia kiatu kipya zaidi ya mara mbili. Hii ilikuwa baada ya kushtumiwa kwa kurudia viatu.

Diamond alidai kwamba kila anapokinunua kiatu hata kiwe cha bei ghali vipi huwa anakivalia mara moja na kisha kukitupa.

" Kuna watu ambao wanasema kwamba mimi hurudia kuvalia viatu, hiyo ni porojo tupu, nina viatu vingi kupindukia na huwa navalia tu mara moja hata kiwe cha bei ghali kivipi, mimi huvitupa ili yule anataka kuvitumia anaweza kuvichukua," alisema Diamond.

Mwaka jana staa huyo wa Bongo alidaiwa kununua ndege ya kibinafsi na kipande cha ardhi katika kisiwa cha Zanzibar.