Diana Marua afichua tabia maalum ya mumewe Bahati ambayo anaipenda zaidi

Bahati alikiri kuwa kwa kawaida yeye humpongeza Diana Marua.

Muhtasari

•Katika video hiyo, mwanamuziki huyo alisifu mlo huo kabla ya kugeuza mada na kuanza kusifia urembo wa mkewe.

•Diana alisema anapenda jinsi mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili huwa anapongeza urembo wake kikweli

Diana Marua na Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Wanandoa Kelvin Bahati na Diana Marua walishiriki mazungumzo ya wazi siku ya Jumatatu jioni walipokuwa wanapata chakula chao cha jioni.

Bahati alichapisha video ya mazungumzo hayo ambapo walikuwa wakizungumzia chakula kizuri ambacho Diana alitayarisha na kumpakulia.

Katika video hiyo, mwanamuziki huyo alisifu mlo huo kabla ya kugeuza mada na kuanza kusifia urembo wa mkewe.

"Mpenzi wewe ni mrembo sana. Kwa nini unaona aibu?" Bahati alimwambia mke wake huku akimwangalia kimahaba.

Ni wakati huo ambapo mama huyo wa watoto watatu alifichua jambo moja la kipekee ambalo anapenda kuhusu mumewe.

Diana alisema anapenda jinsi mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili huwa anapongeza urembo wake kikweli.

"Unajua ninachopenda kukuhusu? Unanipongeza kwa dhati," mwanavlogu huyo alimwambia mume wake.

Aliongeza, "Haijawahi kuwa uwongo.  Wakati mwingine ukikula huwa unanitazama tu na kuniambia, ',mpenzi wewe ni mzuri sana, mpenzi nakupenda. Asante kwa kuwa mke mzuri kwangu."

Bahati alisema kupongezana ni sehemu muhimu ya ndoa na akadokeza kuwa ndiyo siri ya muungano wenye mafanikio.

"Siri ya ndoa, Kupongezana!!" alisema.

Alikiri kuwa kwa kawaida yeye humpongeza Diana Marua na inasaidia kufanya ndoa yao kuwa imara zaidi.

Wakati huohuo, baba huyo wa watoto watano pia  alikiri kuwa amekubali amekubali kutawaliwa na mkewe Diana Marua.

Akizungumza kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu, Bahati alikiri kwa utani kuwa Diana ndiye aliyemuoa.

Aidha, mwanamuziki huyo alibainisha kuwa kukubali kutawaliwa na mke ni jambo nzuri kwa mwanaume.

"Nimekubali, nimekaliwa. Siri ni kukubali kukaliwa," alisema.

Bahati alifichua kuwa hivi majuzi mkewe amekuwa akifika nyumbani jioni sana baada yake, jambo ambalo hana shida nalo.

"Nilikuwa nimelala alafu bibi akarudi. Siku hizi bibi yangu anaingia baada yangu. Niliolewa. Saa hii ameniamsha nikule," alisema chini ya video yake na Diana Marua wakipata chakula chao cha jioni pamoja.

Diana aliweka wazi kwamba alikuwa ametoka kwenye chumba cha mazoezi kabla ya kuingia jikoni kumpikia mumewe.

Bahati ambaye alionekana wazi kufurahia chakula hicho alibainisha kuwa kila siku anataka kula vyakula vilivyopikwa na mkewe.

"Kama hivi ndio napikiwa na mke wangu, nisiwahi kuona Irene amenipikia chakula. Akae na hizo chemsha zake," alisema.