'Haikukusudiwa kuwa, songa mbele na uache yaliyopita yawe!' Amber Ray amsihi ex wake IB Kabba

Amber Ray alikiri kuwa yeye ndiye aliyepiga hatua ya kumwendea Kabba kwa ajili ya mahusiano.

Muhtasari

•Amber Ray amemtaka mpenzi wake wa zamani IB Kabba kuacha kulalamika kuhusu mahusiano yao yaliyogonga mwamba na kusonga mbele na maisha yake.

•Mama huyo wa mvulana mmoja alifichua kuwa alikutana na Kabba hapa nchini Kenya na kujuana kabla ya kuchumbiana.

Amber Ray na aliyekuwa mpenzi wake IB Kabba
Amber Ray na aliyekuwa mpenzi wake IB Kabba
Image: HISANI

Mwanasoshalaiti mashuhuri Faith Makau almaarufu Amber Ray amemtaka mpenzi wake wa zamani kutoka Sierra Leone IB Kabba kuacha kulalamika kuhusu mahusiano yao yaliyogonga mwamba na kusonga mbele na maisha yake.

Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kifupi kabla ya kutengana katika hali tatanishi takriban miezi minne iliyopita. Amber Ray alionekana kuwa sawa na mgawanyiko huo lakini ni wazi kuwa mwenzake bado  hajaweza kuuguza jeraha la moyo.

Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye YouTube channel yake, Amber Ray alibainisha kuwa mahusiano yao hayakukusudiwa kuwa na kumtaka aache kuangazia yaliyopita na badala yake asonge mbele na maisha yake.

"Nataka kuheshimu tulichokuwa nacho lakini haikukusudiwa kuwa. Bwana mchezaji wa mpira wa vikapu, pole sana kama hivyo ndivyo unavyohisi. Tafadhali unaweza kusonga mbele na kuruhusu ya zamani kuwa," Amber Ray alisema.

Mwanasoshalaiti huyo alikuwa akijibu maswali kuhusu maisha yake yenye utata kama yalivyosomwa kwake na Shicco Waweru.

Ingawa hakufichua sababu halisi ya kutengana kwao, Amber Ray alidokeza kuwa huenda kulichangiwa na mizozo mingi iliyotokea kati yao. Alisimulia kisa kimoja ambapo alitofautiana na mwanaspoti huyo baada yao kutoka kujivinjari.

"Tulikuwa na mzozo. Mimi nilikuwa nimelewa, yeye  hakuwa anakunywa pombe. Alichukua simu yangu, tulikuwa kwa nyumba yangu. Kulikuwa usiku sana, hakukuwa na mtu karibu. Nilimwambia aende kwake ningemwongelesha baadae. Hakutaka kuenda, alitaka kuenda na mimi. Kufuatia vita vyetu vya awali sikutaka kuenda naye kwake,"  Alisimulia.

Mama huyo wa mvulana mmoja alifichua kuwa alikutana na Kabba hapa nchini Kenya na kujuana kabla ya kuchumbiana.

Alikiri kuwa ndiye aliyepiga hatua ya kumwendea mchezaji huyo wa mpira wa vikapu kwa ajili ya mahusiano ya kimapenzi.

"Wakati huo nilikuwa single. Nilipomwendea mara ya kwanza nilikuwa wazi, nilimwambia nilichotaka. Sikutaka mahusiano, nilimwambia tujivinjari bila muungano wowote na akakubali," Alisema Amber Ray.

Mwanasoshalaiti huyo alimkosoa Kabba kwa kuendelea kulalamika na kuanika mambo hasi kuhusu mahusiano yao kwenye mitandao ya kijamii na kumtaka aheshimu kipindi kifupi ambacho walishiriki pamoja.