Harmonize afunguka hatari ya kuruhusu mwanamke kwenda gym peke yake kufuatia aliyopitia na Kajala

Harmonize amewaonya wanaume dhidi ya kuwaruhusu wapenzi wao kwenda kwenye gym wenyewe bila kuambatana nao.

Muhtasari

•Harmonize alionya kuwa wanawake wanapokwenda kwenye gym bila wapenzi wao huanza kuwaona wavivu na wasiostahili.

•Konde Boy alisema ushauri wake ulichochewa na yaliyomtendekea hapo awali na mmoja wa wapenzi wake wa zamani.

Image: HISANI

Staa wa bongofleva, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amewaonya wanaume dhidi ya kuwaruhusu wapenzi wao wa kike kwenda kwenye ukumbi wa mazoezi wenyewe bila kuambatana nao.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne jioni, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alionya kuwa wanawake wanapokwenda kufanya mazoezi kwenye gym bila wapenzi wao huanza kuwaona wavivu na wasiostahili.

Alisema kuwa katika hali kama hizi, wanawake kama hao huanza kukagua upya chaguzi zao na kuona kama watu wanaokutana nao kwenye gym kama ndio wanaolingana nao.

“Usiruhusu mpenzi wako kwenda gym mwenyewe kukiwa hakuna sababu za msingi ataanza kuona mzembe na atakaokutana nao kila siku ndio ataanza kuona bora maana wana passion moja!!,” Harmonize alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Aliongeza,”Watabadilishana namba, kesho niamshe, taabu inaanza hapo!! Sio wote lakini, hakikisha kuwa wewe ndiye mkufunzi wake binafsi. Mnishukuru baadaye!!”

Konde Boy alisema ushauri wake ulichochewa na yaliyomtendekea hapo awali, akidokeza kwamba jambo kama hilo lilitokea kwa mmoja wa wapenzi wake wa zamani.

Alidokeza kuwa uhusiano kati ya mwanamke anayeenda gym na mkufunzi wake wa kibinafsi sio wa kuaminiwa kwani lolote linaweza kutokea kati yao.

“Ukaribu wa wakufunzi na mwanafunzi ni mkubwa sana. Lolote laweza kutokea. Hawawezi kumaliza mazoezi bila kumnjoosha viunga, mara mgongo. Sio wote lakini,” alisema.

Bosi huyo wa Kondegang hata hivyo hakushiriki maelezo zaidi kuhusu uzoefu yaliyomtendekea au kufichua ni mpenzi yupi wa zamani aliyemfanya atoe ushauri huo.

Hata hivyo,  kuna uwezekano mkubwa kuwa staa huyo wa bongo fleva alikuwa akimzungumzia mpenzi wake wa hivi majuzi, Fridah Kajala Masanja ambaye ni mpenzi mkubwa wa mazoezi ya viungo.

Kajala huonekena mara kwa mara kwenye ukumbi wa mazoezi na hupenda kushiriki picha na video za vipindi vyake na mkufunzi wake wa kibinafsi.