Harmonize afunguka kuhusu hali yake halisi ya mahusiano, afichua lini atafunga ndoa

Konde Boy alikiri kwamba amewekeza pesa nyingi katika juhudi za kutafuta mapenzi na amani lakini bado hajafanikiwa.

Muhtasari

•Harmonize alikiri kuna mwanamke ambaye ameuteka moyo wake na ambaye anakusudia kuoa iwapo atamkubali.

•Wakati huohuo, Konde Boy alifichua kuwa tayari amepitia matatizo mengi ya kimahusiano mwaka huu,

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amefichua kuwa kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yoyote.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, staa huyo wa bongo fleva hata hivyo alikiri kwamba kuna mwanamke ambaye ameuteka moyo wake na ambaye anakusudia kufunga pingu za maisha naye iwapo atamkubali.

Harmonize alisema kuwa mwanamke huyo ambaye hakufichua jina lake ni mwanamke wa ndoto zake na akadokeza kuwa yuko tayari kumfanya kuwa mke wake.

“Sipo kwenye mahusiano!! Ila kuna mtoto nampenda sana!! Akisema Ndiyo!! Naoa Kabisa!! SHE IS MY DREAM GIRL!!,” Harmonize alisema kupitia Instagram.

Msanii huyo wa zamani wa WCB alibainisha kuwa siku zote alikusudia kuoa baada ya kufikisha umri wa miaka 30, kupata pesa za kutosha, kupata furaha, afya njema na mwanamke wa ndoto zake. Mambo ambayo anahisi anakaribia kutimiza.

“Machi 15, 2024 natimiza 30 Inshallah. Kifupi kabakia yeye tuu. Nikizungumzia msichana mrembo zaidi wa Tanzania unayemfahamu,” alisema.

Wakati huohuo, Konde Boy alifichua kuwa tayari amepitia matatizo mengi ya kimahusiano mwaka huu, mengine yaliyo hadharani huku mengine yakiwa ya faragha.

Alikiri kwamba amewekeza pesa nyingi katika juhudi za kutafuta mapenzi ya kweli na amani lakini bado hajafanikiwa.

“Hela nilizowekeza kwenye mahusiano ingalikuwa nampatia mwanamke mmoja wa Tanzania, bila shaka tungeshakuwa na dada mjasiriamali bora kabisa Mtanzania!! Ama ningewekeza kwenye kitu kingine katika uwekezaji wangu chenye thamani. Ila niliamini katika furaha yangu, maana siku zote my peace of mind comes first,” Harmonize alisema.

Aliongeza, “Napenda kuwa mwenye furaha ili niendelee kuwahudumia na muziki bora!! Pia nipate muda wa kutengeneza afya bora! Na ndio maana chochote kinachohusisha amani ya moyo wangu nakipa moyo.

Mwimbaji huyo mahiri alikiri kuwa amejaribu hata kutafuta mapenzi nje ya nchi yake ya Tanzania lakini bado hajampata mwanamke ambaye yuko tayari kumalizana naye.

Hata hivyo alidokeza kuwa huenda hatimaye amepata alichokuwa akitafuta kwa udi na uvumba na kusema kwamba atashiriki habari za kufurahisha na mashabiki wake hivi karibuni.