Harmonize avuruga urafiki na Hamisa Mobetto baada ya kumtishia mpenzi wake Kevin Sowax

Mastaa hao wameacha kufuatiliana kwenye mtandao wa Instagram ambako walikuwa wakitangaza urafiki wao mkubwa.

Muhtasari

•Ni wazi kuwa huenda mambo sio sawa tena kati ya waliokuwa marafiki wakubwa, Harmonize na mwanamitindo Hamisa Mobetto.

•Harmonize alizungumza vibaya kuhusu mpenzi wa mwanamitindo huyo akijigamba kuwa tajiri kuliko yeye kwa mbali sana.

Harmonize ametupa vijembe kwa mumewe Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM

Kuna uwezekano mkubwa kuwa mambo sio sawa tena kati ya waliokuwa marafiki wakubwa, Harmonize na mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Hii imeonyeshwa na maendeleo ya hivi punde ambapo wote wawili wameacha kufuatiliana kwenye mtandao wa Instagram au hata kufungiana. Walikuwa wakifuatiliana kwa muda mrefu na hata kutajana mara kwa mara kuonyesha urafiki wao.

Hatua hii imekuja siku chache baada ya mpenzi wa Hamisa Mobetto, Kevin Sowax kuwasili nchini Tanzania kwa mara ya kwanza na kukiri kuwa hata hamfahamu bosi huyo wa Konde Music Worldwide ambaye anadai kuwa rafiki mkubwa wa mpenzi wake.

"Simjui, simjui," Kelvin alisema katika mahojiano wakati alipoulizwa ikiwa anafahamu urafiki wa Harmonize na mpenzi wake.

Ugomvi kati ya Hamisa na Harmonize huenda ulishika moto siku ya Alhamisi baada ya bosi huyo wa Kondegang kuzungumza vibaya kuhusu mpenzi wa mwanamitindo huyo akijigamba kuwa tajiri kuliko yeye kwa mbali sana.

wameacha kufuatiliana kwenye Instagram.
Harmonize na Hamisa Mobetto wameacha kufuatiliana kwenye Instagram.
Image: INSTAGRAM

Wakati akijibu madai ya mtangazaji Juma Lokole kwamba hawezi kushindana na Kevin katika masuala ya fedha, Konde Boy alisema kuwa mifuko yake imesheheni zaidi ya Mtogo huyo.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alidokeza kuwa njia mojawapo ya kulinganisha utajiri wao ni kuangalia aina ya gari kila mmoja anamiliki.

“Ingawa mimi sio mtu wa kuongelea maisha ya watu nisiowajua lakini niamini niko na hela nyingi kuliko jamaa huyo. Kabla hujamnunulia mwanamke gari inatakiwa tujue unaendesha gari ganii!! Au ndio hayanihusu. Si tushavuka kwenye magari,” Harmonize alisema katika taarifa kwenye Instastori zake.

Ili mfanyibiashara huyo wa Togo kudhihirisha kuwa yeye ni tajiri sana kama inavyodaiwa, Harmonize amemtaka amnunulie Hamisa nyumba.

"Kama hawezi, basi nitamuonyesha jinsi tulivyo serious na marafiki zetu wakubwa, sisi wanaume wa Kitanzania!! Kwenye magari tushavuka,” alisema.

Wakati huo huo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alisisitiza kuwa mpenzi huyo wa zamani Diamond Platnumz ni rafiki yake tu na si mpenzi wake.

Hivi majuzi, Hamisa Mobetto alikanusha madai ya kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Harmonize.

Kwenye mahojiano na Rick Media, mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz alibainisha kuwa hakuna chochote kikubwa kati yake na Konde Boy na kubainisha kuwa mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ ni rafiki yake tu.

“Yeye ni rafiki tu. Hakuna zaidi, hakuna kidogo, "alisema.

Baada ya kubainishiwa kuwa Harmonize anayapenda sana makalio yake makubwa, mama huyo wa watoto wawili alikiri kuwa hafahamu hilo.