"Hawawezi kubali nilale soko ata siku moja!" Karen Nyamu ajigamba huku akijibu kuhusu kuwa single

Seneta huyo wa kuteuliwa alidai kuwa wanaume hawawezi kumruhusu hata kidogo akae bila mpenzi.

Muhtasari

•Bi Nyamu alisema hayo alipokuwa akimjibu mwanamtandao  aliyeibua madai kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa yeye ni single sasa.

•“Mimi hawawezi kubali nilale soko ata siku moja,” Bi Nyamu alijibu.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Wakili na seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amedokeza wazi kuwa si rahisi kwa yeye kuwa bila mchumba.

Mama huyo wa watoto watatu alisema hayo alipokuwa akimjibu mwanamtandao ambaye aliibua madai kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa yeye ni single sasa.

Siku ya Jumapili asubuhi, mtumiaji wa mtandao wa Facebook, Anne Dadou, alidai kuwa hatua ya Bi Nyamu kuvaa nadhifu zaidi katika siku za hivi majuzi  huenda ilichochewa na ukweli kwamba anatafuta mpenzi.

“Ukiona mtu ameanza kupiga luku sana jua tu ako single,” Anne aliandika chini ya moja ya posti za Karen Nyamu kwenye Facebook.

Katika majibu yake, seneta huyo wa kuteuliwa alidai kuwa wanaume hawawezi kumruhusu hata kidogo akae bila mpenzi.

“Mimi hawawezi kubali nilale soko ata siku moja,” Bi Nyamu alijibu.

Hali ya sasa ya mahusiano ya mwanasiasa huyo mwenye utata imesalia kuwa kitendawili katika miezi michache iliyopita, na kuwaacha watu kukisia tu.

Kwa muda sasa, hajatangaza wazi wazi mapenzi yake na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, kama alivyokuwa akifanya hapo awali. Hili limezua wasiwasi miongoni mwa wafuasi wake, wengine wakiamini kuwa uhusiano wao wa miaka mingi unaweza kuwa umeisha.

Bi Nyamu na baba huyo wa watoto wake wawili pia hawajaonekana pamoja kwa muda mrefu sasa, kama walivyokuwa wakionekana hapo awali.

Mapenzi ya hadharani kati ya wazazi wawili hao yalionekana kupungua kuanzia takriban miezi mitatu iliyopita wakati Samidoh alipofunga safari hadi Marekani kumtembelea mke wake wa kwanza Edday Nderitu na watoto wao watatu. Wawili hao walionekana kuwa na wakati mzuri huko na familia yao.

Katika picha na video ambazo zilirekodiwa  nchini Marekani mwezi Juni,  wazazi hao wawili walionekana kuwa na furaha pamoja na kushikana kama watu wanaopendana.

Hii ilibua tena maswali tata kuhusu hali halisi ya ndoa ya wawili hao ambao waliishi pamoja kwa zaidi ya muongo mmoja hadi mwaka jana wakati ambapo Edday pamoja na watoto wao watatu walihamia Marekani na kumuacha Samidoh nchini Kenya.

Bi Edday Nderitu kwa sasa anaishi Marekani pamoja na watoto wao watatu.  Aliondoka nchini mapema mwaka jana na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.