"Hili litapita kama mengine!" Diamond amfariji Manara baada ya kutemwa na mkewe wa pili

Staa huyo amewasuta wale ambao wamekuwa wakimkejeli Bw Manara.

Muhtasari

•Manara amekuwa akionekana na mke wake wa kwanza pekee, tofauti na hapo awali ambapo alikuwa akijigamba na wake zake wote wawili.

•Diamond ameeleza kusikitishwa kwake na watu ambao wamekuwa wakifanya mzaha na kuvunjika kwa ndoa ya Manara.

Haji Manara na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// HAJI MANARA

Bosi wa WCB Diamond Platnumz amemliwaza msemaji wa klabu ya Yanga SC nchini Tanzania , Haji Manara kufuatia madai ya kuachwa na mke wake wa pili.

Siku za hivi karibuni, Manara amekuwa akionekana na mke wake wa kwanza pekee, tofauti na hapo awali ambapo alikuwa akijigamba na wake zake wote wawili. Duru za kuaminika zinaarifu kwamba mke wake wa pili, Rushaynah, amemtema

Diamond sasa amemtia moyo afisa huyo wa soka nchini Tanzania ambaye amekuwa akifanya naye kazi kwa karibu siku za hivi karibuni na kumfahamisha kuwa chochote anachokipitia kwa sasa ni dhoruba ambayo itapita hivi karibuni.

"Kaka yangu Haji Manara, hili nalo litapita kama mengine yalivyo kwendaga, na kwa ninavyojua ata presha huna, maana sana sana limetuongezea upeo, umaarufu na deals za endorsment kwa kuzungumziwa na nchi 24/7," alisema kwenye Instagram.

Aidha, staa huyo wa Bongo ameeleza kusikitishwa kwake na watu ambao wamekuwa wakifanya mzaha na kuvunjika kwa ndoa ya Manara.

Alibainisha kuwa watu kuzungumza sana kuhusu masaibu yaliyompata Manara kunaaashiria tu kuwa walikuwa wakiionea gere ndoa yake.

"Ushadadi na Tafrija za baadhi ya watu juu ya mtihani wa ndoa ya bugati, unaonesha ni kiasi gani walivyokuwa na wivu na husda na ndoa zake, utazani labda wao walizuiwa kuoa ama kuolewa vile!," alisema.

Kwa wiki kadhaa, Manara ambaye alikuwa akionekana na wake zake wawili kila sehemu alianza kuonekana na mke wa kwanza tu huku wengi wakiibua maswali kuhusu uwepo wa mke wa pili kwa jina Rushaynah.

Awali, Manara mwenyewe aliwaaminisha wadadisi hao kuwa Rushaynah alikuwa mgonjwa na ndio maana hakuwa anaonekana naye kama awali.

Baadae hata hivyo, mashaka miongoni mwa waliokuwa wakifuatilia ndoa yao yaliendelea kupanda hasa baada ya kubainika kuwa hawafuatani tena kwenye mitandao ya kijamii kama ilivyokuwa hapo awali.

Kitendo hicho kilidhibitisha kwa asilimia kubwa kuwa huenda Rushaynah amejiondoa katika ndoa hiyo ya utatu na katika blogu moja ambayo ilipakia video ya zamani wakichezeana na Manara, Rushaynah mwenyewe alifika pale na kutaka video ile iondolewe mara moja kwani kwa kuiona tu anachefuka.

Blogu ya bongotrending inachapisha video hiyo na kuinukuu, “Manara na pisi lake.”

Rushaynah kwa haraka mno alifika pale na kutoa tamko lililowaacha wengi katika maswali mengi akisema,“wewe koma, hebu futa.”

Kama hilo bado halijapoa, usiku wa kuamkia Jumanne, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram aliachia ujumbe mrefu akimuomba msamaha mke wake wa kwanza Rubi kwa kumletea mke wa pili huku pia akimtakia kila la kheri katika safari yake ya ujauzito na kujifungua salama.

Manara alisema pamoja na mke wake wa kwanza, wamedumu kwenye ndoa kwa miaka 7.