"Huba limetaradadi" Diamond Platnumz afunguka kuhusu mahusiano yake mapya

Muhtasari

•Diamond alikiri kwamba mahusiano yake mapya yamejawa na mahaba kochokocho na anayafurahia kila siku.

•Aliweka wazi kuwa anampenda sana malkia anayechumbia kwa sasa huku akidhihirisha kuwa anayathamini mahusiano yao.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Gwiji wa Bongoflava Naseeb Abdul Juma almaarufu kama Diamond Platnumz  amefichua kwamba tayari  amepata penzi tena na kwa sasa yuko kwenye mahusiano.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media usiku wa Valentine's, Diamond alikiri kwamba mahusiano yake mapya yamejawa na mahaba kochokocho na yanampa raha kubwa.

"Niko kwenye mahusiano. Nina furaha. Nafurahia, mahusiano yangu yananipa raha na amani. Huba limetaradadi, mahaba ndi ndi ndi" Diamond alisema.

Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana hata hivyo hakufichua jina wala chochote kuhusu mpenzi wake wa sasa.

Aliweka wazi kuwa anampenda sana malkia anayechumbia kwa sasa huku akidhihirisha kuwa anayathamini mahusiano yao.

"Nampenda sana. Yeye anafahamu nampenda. Maneno tupu hayatoshi, ila matendo yangu anayaona" Diamond alisema.

Diamond anaaminika kuwahi kuchumbia zaidi ya wanawake kumi kutoka mataifa mbalimbali na kuzaa watoto na angalau watatu wao.

Miaka ya hivi karibuni mwanamuziki huyo amechumbia wasanii Hamisa Mobetto na Wema Sepetu kutoka Tanzania, mwanasoshalaiti Zari Hassan kutoka Uganda na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya.

Hivi majuzi kumekuwa na uvumi kwamba huenda bosi huyo wa WCB anachumbia msanii wake Zuchu, jambo ambalo sasa limethibitishwa sio kweli.