Huku penzi la Harmonize na Kajala likinoga, aliyekuwa mpenziwe apanga harusi na mchumba wake

Wolper anapanga kufunga pingu za maisha na mchumba wake Rich Mitindo mwezi ujao.

Muhtasari

•Wolper na Mitindo waliweka bango kubwa kando ya barabara moja kuu ya Tanzania kutangaza tarehe ya harusi yao.

•Rich Mitindo alimvisha Wolper pete ya uchumba mnamo Agosti 2021.

Wolper na Mchumba wake Rich Mitindo
Image: INSTAGRAM// RICH MITINDO

Aliyekuwa mpenzi wa Harmonize,Jacqueline Wolper  anapanga kufunga pingu za maisha na mchumba wake Rich Mitindo mwezi ujao.

Wolper na Mitindo waliweka bango kubwa kando ya barabara moja kuu ya Tanzania kutangaza tarehe ya harusi yao.

Mama huyo wa watoto wawili alitangaza kuwa hafla ya harusi yao itapeperushwa moja kwa moja kwenye stesheni maarufu ya TV ya Tanzania.

“Nyie naolewa mjue. Alafu sasa  naolewa na kiboko yangu. Haya mambo yameiva tunayo na tunaanza na singo 04/11” alisema kupitia Instagram.

Rich Mitindo alimvisha Wolper pete ya uchumba mnamo Agosti 2021.

"Hakuna kitu kizuri kama kuchumbiwa na mwanamume unayempenda. Mungu ametimiza ahadi yake ya pili baada ya kupata mtoto," Wolper alisema wakati huo.

"Nimesikia watu wakisema kwambana nachumbiwa kwa mara ya nne au la tatu sasa, na bado nimelia. Ndiyo, nililia sana hata nililia zaidi nilipofika nyumbani."

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize pia alikanusha madai ya kumnunulia pete Rich ili amchumbie.

Wenzi hao walikutana mwaka wa 2016 lakini wakatengana kwa muda baada ya miaka miwili.

Wolper alikiri kuwa yeye ndiye aliyemkosea Mitindo kabla na kusababisha kutengana kwao.

Baadaye walipatana mwaka wa 2020, wakati ambapo wote walikuwa single tena, na wakajitosa kwenye mahusiano.

Wakati wachumba hao walipokuwa wametangana, Wolper alikutana na Harmonize na kuchumbiana kwa takriban mwaka mmoja kabla ya kutengana katika hali tatanishi.

Baada ya kutengana kwao mwaka wa 2017, Wolper alidai kuwa alitoka kwenye mahusiano hayo kwa sababu Harmonize alikuwa akitoka kimapenzi na mwanamke mwingine.

Katika utetezi wake basi, Wolper alimshutumu staa huyo wa Bongo kwa kuchunguza simu yake na kutafuta uchafu. 

Harmonize hata hivyo alijitokeza kupinga madai ya Wolper  na kumnyooshea muigizaji huyo kidole cha lawama akidai kuwa alimcheza na wanaume wawili.

Baada ya kutengana, Harmonize alijitosa kwenye mahusiano na Sarah Michelloti kabla ya wao kutengana mwaka wa 2020.

Staa huyo wa Bongo kwa sasa yupo kwenye mahusiano ya kimapenzi na muigizaji Frida Kajala Masanja na tayari amemvisha pete ya uchumba mama huyo wa binti mmoja.