J Blessing hatimaye avunja kimya baada ya mpenzi wake Avril kumshtumu kwa kumpiga

Producer huyo ametangaza kwamba yeye na Avril wamekubali kuishi tofauti baada ya tukio la wasiwasi la hivi punde.

Muhtasari

• J Blessing alidai kuwa moja ya picha alizochapisha mzazi mwenzake huyo ni tukio lililotokea mwaka jana.

•Jumanne usiku, Avril aliposti picha zake akiwa na michubuko usoni na kudokeza J Blessing alimvamia na kumpiga.

amevunja kimya baada ya Avril kumshutumu kwa kumpiga.
J blessing amevunja kimya baada ya Avril kumshutumu kwa kumpiga.
Image: HISANI

Mtayarishaji wa muziki maarufu wa Kenya J Blessing amekiri kuwa kulikuwa na ugomvi uliomhusisha yeye na mzazi mwenzake Judith Nyambura almaarufu Avril.

Hii ni baada ya malkia huyo wa muziki kushiriki picha za kutisha za uso wake wenye alama za kushambuliwa na kusema maneno makali dhidi ya babake mwanawe.

Huku akijibu tuhuma za dhuluma zilizotolewa na mzazi mwenzake, J Blessing alikana kumpiga mwanamuziki huyo na kueleza kuwa haungi mkono vurugu.

“Habari za mchana. Ndiyo, tulikuwa na ugomvi hadharani, lakini haukuhusisha kumpiga kama ilivyopendekezwa. Siungi mkono aina yoyote ya vurugu,” J Blessing alisema baada ya kutafutwa na Mpasho kwenye Instagram.

Katika maelezo mengine, J Blessing alidai kuwa moja ya picha alizochapisha mzazi mwenzake huyo ni tukio lililotokea mwaka jana.

Alikiri kuwa walikuwa na ugomvi uliosababisha kupigana, na kusababisha majeraha kwa wote wawili ambayo yalitibiwa hospitalini.

“Naomba radhi sana kwa madhara niliyomsababishia Avril au mtu mwingine yeyote. Nina hatia, lakini ningependa kufafanua mambo machache. Karibu mwaka mmoja uliopita, tulikuwa na ugomvi wa kimwili ambapo sote tulijeruhiwa, na siku hiyo, mara moja nilimpeleka hospitali. Ninachukua jukumu kamili kwa wakati huo wa udhaifu. Moja ya picha alizoweka ni za tukio hilo,” J bless alisema.

Aliongeza, “Jana usiku kulitokea hali iliyosababisha ugomvi, lakini haikuwa kipigo kama ilivyopendekezwa. Ninataka kumhakikishia kila mtu kwamba sikumpiga. Mimi si mnyanyasaji, na sikumpiga. Mimi ni binadamu ambaye nilifanya makosa katika maisha yangu."

Mtayarishaji huyo pia alitangaza kuwa yeye na Avril wamekubali kuishi tofauti baada ya tukio la hivi majuzi lililowahusu.

Mnamo Jumanne usiku, Avril alichapisha picha zake akiwa na michubuko usoni na kudokeza kuwa baba ya mwanawe alimvamia na kumpiga.

Baadaye, mwimbaji huyo alijitokeza kujitetea na kueleza kwa nini alifikia kufunguka hadharani kuhusu yale aliyokuwa akipitia faragha.

"Siku zote nimekuwa mtu wa faragha sana. Siwezi kamwe kuzungumza kuhusu chochote ninachopitia hata kama ninateswa nacho,” Avril alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram Jumatano asubuhi.

Aliendelea, “Moyo wangu ni mzito sana hivi kwamba ilinibidi kuuambia ulimwengu mambo yangu. Ndiyo, niliona kejeli kuhusu mimi kustahili kila kitu ambacho nimepitia enzi za uhai wangu na nina hakika kutakuwa na kejeli zaidi, lakini pia niliona jumbe za upendo na usaidizi."

Mama huyo wa mtoto mmoja ziadi aliweka wazi kuwa amemsamehe J Blessing kwa lolote lililotokea kati yao na pia kuwataka mashabiki wake wamsamehe mzazi mwenzake huyo.

"Ninakubali kwamba uhusiano wetu wa miaka saba na safari yetu kama wazazi kwa mvulana mdogo mzuri imekabiliwa na changamoto, na kumekuwa na migogoro ambayo iliongezeka hadi mapigano. Tunatambua hitaji la mabadiliko na tumejitolea kutafuta usaidizi na kujifunza njia bora za kuwasiliana na kutatua masuala. Lengo letu la pande zote mbili ni kujenga mazingira chanya na kusaidiana zaidi, kukuza uelewano na ukuaji,” alisema.

Pia aliweka wazi kuwa hakuwa akifuatilia suala hilo, kama baadhi ya wanamtandao wa Kenya walivyodai.