Jiandaeni! Yesu wa Tongaren atabiri siku ambayo dunia itaisha

Alisema kwamba farasi wa ajabu atatokea na watu watatoweka wakimtazama.

Muhtasari

•Bw Wekesa anayedai kuwa Yesu Kristo halisi alidai kuwa Mungu anapanga kumaliza kizazi cha sasa katika mwaka wa 2058.

•Nabii huyo mwenye utata alidai kwamba Mwenyezi Mungu atawamaliza watu kama vile alivyofanya na Sodoma na Gomora.

Yesu wa Tongaren
Image: HISANI

Nabii wa Kenya mwenye utata Eliud Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren ametabiri tukio kubwa litakalotokea duniani katika muda wa takriban miongo mitatu ijayo.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Bw Wekesa anayedai kuwa Yesu Kristo halisi alidai kuwa Mungu anapanga kumaliza kizazi cha sasa katika mwaka wa 2058.

Alisema kwamba farasi wa ajabu atatokea na watu watatoweka wakimtazama.

“Kulingana na hali ya dunia kuisha, ukisoma Isaya 24 hapo, utaelezewa tu Mwenyezi Mungu atausokota uso wa dunia,” Yesu wa Tongaren alisema.

Aliendelea, “Dunia yenyewe haiishi, ila tu kizazi hiki ambapo Mungu ameweka katika uso wa dunia kitaisha kuanzia mwaka huu kuendelea. Kila jicho litamtazama farasi aliye na mtwara kichwani na kutoweka, ile hali niliambiwa itakuwa 2058. Lakini sio eti dunia kuisha, watu wataisha.”

Nabii huyo mwenye utata alidai kwamba Mwenyezi Mungu atawamaliza watu kama vile alivyofanya na Sodoma na Gomora.

Hata hivyo alidai kuwa yeye hatakuwa miongoni mwa watu wa kuangamizwa kwani kulingana na yeye, atapata uzima wa milele.

“Mimi ni wa uzima wa milele. Nilikuwa na yeye kutuka mwanzo,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuwasihi Wakenya kuwa waangalifu zaidi na akaomba Mungu awasaidie kufungua macho yao kuona kinachoendelea.

Katika mahojiano ya mapema mwaka jana na Massawe Japanni, Bw Simiyu alifunguka kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake.

Katika mahojiano hayo, Bw Simiyu alifichua kwamba hakwenda mbali na masomo yake. 

Mzee huyo kutoka Bungoma anayedai kuwa yeye ni Yesu Kristo ambaye amerudi duniani kwa mara ya pili  ili kuwakomboa Walimwengu alibainisha kuwa Biblia haisemi kuhusu historia ya masomo ya Yesu.

"Kwa Biblia mliona wapi historia ya Yesu ya kusoma?"  Simiyu alihoji alipoulizwa kuhusu kiwango cha masomo yake.

Baba huyo wa watoto wanane alifichua kwamba alifaulu tu kusoma hadi kidato cha kwanza na baada ya hapo hakuweza kuendelea.

Simiyu alisema licha ya kutosoma sana alifanikiwa kupata kazi maalum ya kuwakomboa walimwengu ambayo anaifurahia.

"Mimi sikusoma masomo ya ulimwengu sana. Nilifika katika darasa la nane. Nilijiunga na shule ya upili lakini nikabaki kidato cha kwanza. Namshukuru Mungu kwa hii kazi yangu," alisema.

Licha ya kutokuwa na elimu kubwa, Bw Simiyu alibainisha kuwa ameweza kutembelea mataifa yote duniani kiroho.

"Saa hii nimezunguka mataifa yote ya dunia kiroho na hata walimwengu wananitazama sasa kwenye runinga," alisema.

Alifichua kuwa alizindua kanisa lake 'Kanisa la Yesu' mwaka wa 2009 na ameendeleza  injili kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alisema kuwa kanisa lake lina manabii kumi na wawili pamoja na washirika wengine.