Jimal Rohosafi afichua sababu kuu ya kufanyiwa utaratibu wa kupandikiza nywele

Mfanyabiashara huyo wa matatu alibainisha kuwa kupandikiza nywele ni njia ya kujionyesha upendo.

Muhtasari

• Rohosafi amedokeza kuwa tamanio la kubaki kijana milele ndiyo sababu inayompa shinikizo la kufanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa nywele.

•Jimal pia amefichua kuwa mbali na kupandikizwa nywele pia ana mpango wa kufanyiwa utaratibu maalum wa kupunguza uzito wa mwili.

Image: INSTAGRAM// JIMAL ROHOSAFI

Mfanyabiashara mashuhuri wa Kenya Jimal Marlow Rohosafi amedokeza kwamba tamanio la kubaki kijana milele ndiyo sababu inayompa shinikizo la kufanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa nywele.

Siku ya Jumanne, Jimal ambaye kwa sasa yuko nchini Uturuki kwa sehemu ya pili ya upandikizaji wa nywele zake alionyesha video ya mhudumu wa hospitali akimhudumia.

Chini ya video hiyo aliyochapisha Instagram, baba huyo wa watoto watatu alisema kuwa ni ndoto ya kila mtu kutozeeka.

"Ndoto ya binadamu wote ni kukaa mchanga milele," Jimal aliandika chini ya video aliyopakia kwenye mtandao wa Instagram.

Aliambatanisha video hiyo na wimbo wa ‘Young Forever’ wa Jay-Z na Mr Hudson.

Katika chapisho lingine, mfanyabiashara huyo wa matatu alibainisha kuwa kupandikiza nywele ni njia ya kujionyesha upendo.

"Daima jipende mwenyewe kwanza," aliandika chini ya picha ya kichwa chake ambayo alichapisha.

Jimal pia amefichua kuwa mbali na utaratibu wa kupandikiza nywele pia ana mpango wa kufanyiwa utaratibu maalum wa kupunguza uzito wa mwili wake.

"Ninahitaji kupungua kutoka kilo 95 hadi 75 katika miezi 4. Leo ni Allurion Intragastric Balloon: Hatua kwa hatua,” aliandika.

Jimal aliratibiwa kufanyiwa utaratibu wa kupandikizwa nywele katika siku za nyuma lakini akaahirisha kwa sababu ya COVID.

"Naenda kwa sehemu ya pili. Ya mwisho," alitangaza akiahidi kushiriki kabla na baada ya picha.

Uturuki inasemekana kuwa kitovu cha taratibu mbalimbali za urembo. Aliyekuwa mke wa Jimal, Amira pia aliwahi kusafiri huko kwa ajili ya utaratibu wa kupunguza uzito wa mwili.

Taratibu za kupandikiza nywele huwa na gharama ya takriban $4,500 (Sh 664,920). Kupandikiza nywele nchini Uturuki kunahusisha kuondoa nywele kutoka kwa eneo la wafadhili (kawaida nyuma ya kichwa, lakini pia ndevu na maeneo mengine ikiwa ni lazima) na kupandikiza.