Jimal Rohosafi azungumzia maendeleo ya afya baada ya kuugua hadi kulazwa hospitalini

Mfanyibiashara huyo amefichua kuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Muhtasari

•Jumatatu asubuhi mfanyibiashara huyo alizua wasiwasi mitandaoni baada ya kufichua kuwa alilazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla.

•Jimal sasa amesema kuwa afya yake tayari imerejea kikamilifu na kufichua kuwa  ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Jimal Rohosafi
Image: Instagram

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki Matatu jijini Nairobi Jimal Marlow Rohosafi ameweka wazi kuwa sasa yupo sawa baada ya kuugua mapema wiki hii.

Jumatatu asubuhi mfanyibiashara huyo alizua wasiwasi mitandaoni baada ya kufichua kuwa alilazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla.

Jimal alieleza kwamba alishambuliwa na ugonjwa usiothibitishwa muda mfupi tu baada ya kuondoka kazini Jumapili usiku.

"Nachukia hospitali.. sekunde chache tu baada ya kutoka ofisini.. Nilihisi kuwa siko sawa, kila kitu kitakuwa sawa," Jimal alitangaza Jumatatu asubuhi kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Baba huyo wa watoto wawili   aliambatanisha ujumbe wake na picha iliyoonyesha akiwa amelala kwenye kitanda cha hospitali na kudokeza kuwa alilazwa mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Jumatatu.

Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi  wala kufichua ugonjwa ambao ulimuathiri hadi kufikia hatua ya kulazwa.

Jimal sasa amesema kuwa afya yake tayari imerejea kikamilifu na kufichua kuwa  ameruhusiwa kutoka hospitalini.

"Alhamdullah.. Nipo sawa sasa. Shukran nyote kwa kunijulia hali. Sasa tupo site!" Jimal alitangaza Jumanne kupitia Instastori zake.

Mfanyibiashara huyo pia alipakia picha zake kadhaa  za sasa zilizoonyesha akiwa mchangamfu na  buheri wa afya.

"Sio kila wakati kuhusu mali !! Baadhi ya watu wanaona wivu juu ya utu wako, nguvu zako na jinsi watu wengine wanavyokupenda.. 100% afya nzuri, afya ni mali, tabasamu zaidi," Aliandika chini ya picha alizopakia.

Jimal amezungumziwa sana mitandaoni katika  kipindi cha takriban mwaka mmoja ambacho kimepita huku wanamitandao wakiangazia ndoa yake.

Wiki kadhaa zilizopita mfanyibiashara huyo alipiga hatua ya kuomba msamaha kutoka kwa mkewe kwa kualika drama nyingi kwenye ndoa yao ya miaka mingi.

Ndoa ya Jimal ilianza kusambaratika mwaka jana baada ya kujitosa kwenye mahusiano na mwanasoshalaiti Amber Ray.

Amber Ray kwa sasa yupo kwenye mahusiano mengine huku Jimal akihangaika kumrejesha nyumbani mkewe Amira.