Jinsi Bahati anapanga kuhakikisha watoto wake wanaonja maisha magumu aliyopitia

Bahati amekuwa akijitahidi sana kuwapa maisha laini, jambo ambalo hakubahatika kuwa nalo wakati akikua.

Muhtasari

•Bahati alifichua kwamba watoto wake Heaven na Majesty wameacha kupelekwa shuleni na dereva wao na sasa wanabebwa na basi la shule kama watoto wengine wengi.

•Alisema anapanga kuwaacha wapande matatu na hata kutembea hadi shuleni, katika hatua ya kuhakikisha kwamba wanaonja ugumu wa maisha.

na watoto wao Majesty na Heaven Bahati.
Bahati, mkewe Diana Marua na watoto wao Majesty na Heaven Bahati.
Image: HISANI

Mwimbaji Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefichua kuwa yuko kwenye dhamira ya kuhakikisha kuwa watoto wake wanapata kuonja maisha magumu kama aliyopitia wakati akikukua.

Siku ya Jumatatu, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alifichua kwamba watoto wake wawili wadogo, Heaven na Majesty Bahati wameacha kupelekwa shuleni na dereva wao na sasa wanabebwa na basi la shule kama watoto wengine wengi.

Pia alitangaza kuwa hivi karibuni anapanga kuwaacha wapande matatu na hata kutembea hadi shuleni, katika hatua ya kuhakikisha kwamba wanaonja ugumu wa maisha.

“Watoto wangu walikuwa wamezoea kupelekwa shule na dereva kwenye Prado.Sasa nimewaweka Kwa Basi la Shule… Mara hiyo nyingine nataka nifanye mpango wakuwe wanatumia matatu mara mbili kwa wiki alafu wanaenda mguu mara moja kwa mwezi 😂 🙈😀😂 Lazima waonje Maisha ambayo Nimepitia #TheBahatis 😎,” Bahati alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na video yake akiwa na mkewe Diana Marua wakiwasindikiza Heaven and Majesty hadi kwenye basi la shule lililokuwa limesimama getini kwao.

Bahati amekuwa akiwalea watoto wake kwa njia tofauti kabisa na jinsi alivyolelewa. Amejitahidi kuwapa maisha laini, jambo ambalo hakubahatika kuwa nalo wakati akikua.

Mwanamuziki huyo mashuhuri alimpoteza mama yake mzazi akiwa na umri mdogo wa miaka saba. Baada ya mama yake kufariki, mwanamuziki huyo alichukuliwa na ABC Children's Home ambako alilelewa.

Takriban miaka miwili iliyopita, Bahati alifunguka kuwa mama yake alifariki mnamo siku ya Krismasi ndani ya nyumba  akisubiri zamu yake ya kuhudumiwa hospitalini. Wakati huo Bahati alikuwa na umri wa miaka sita.

"Kulikuwa na hospitali moja tu ndogo katika eneo la Mathare. Wiki ambayo mamangu alifariki, hata mimi niliwahi kuamka na mtu saa tisa usiku ili tukampangie foleni hospitalini. Hivyo ndivyo mamangu alivyofariki. Mama yangu alikufa wakati mtu mwingine akiwa  amempigia foleni hospitalini," Bahati alisimulia akiwa kwenye mazungumzo na mkewe Diana Marua.

"Alifariki mida ya adhuhuri. Akakaa kwa nyumba kwa masaa kadhaa. Alasiri ilipofika mwili wake ulikuwa umefungwa kwenye blanketi, tukakodishwa teksi ili tumpeleke mochari" Aliendelea.

Bahati alieleza kuwa hatua ya kumpoteza mamake ilikuwa pigo kubwa kwake na ilimbadilishia maisha sana.

"Nilidhani maisha yangu Nairobi yameisha. Nilijua baada ya maziishi ningepelekwa kuishi Ukambani. Huo ndio ulikuwa mpango. Tulikuwa maskini. Baba yangu hangeweza kumudu sisi kuwa na kijakazI... Nilidhani maisha yangu yameisha. Baada ya mazishi nililia sana ili nisiachwe. Nilijificha kwenye gari iliyokuwa imebeba mwili.Nilianza kuishi na jirani," Bahati alisema.

Baadae, mwanamuziki huyo alienda kuishi kwenye Children's Home hadi alipotimiza umri wa kujisimamia.