Jinsi dadake Diamond alivyodhibiti ndoa yake na Msizwa

Msizwa alidai ilikuwa wazo na uamuzi wa Esma kuvunja ndoa yao ya muda mfupi.

Muhtasari

•Msizwa alidai kuwa dada huyo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz aliomba kusitiliwa na kufadhiliwa.

•Pia alidokeza kuwa Esma kisheria bado ni mke wake kwa sababu bado hawatalikiana.

Mfanyibiashara Yahya Msizwa na dadake Diamond, Esma Platnumz.
Image: HISANI

Mfanyibiashara bwenyenye wa Tanzania Yahya Msizwa amesisitiza kuwa Esma Platnumz ndiye aliyemwomba amchukue awe mke wake. 

Katika mahojiano na waandishi wa habari, Msizwa alidai kuwa dada huyo wa staa wa Bongo Diamond aliomba kusitiliwa na kufadhiliwa.

Mfanyabiashara huyo pia alidai kuwa pia ilikuwa wazo na uamuzi wa Esma kuvunja ndoa yao ya muda mfupi.

"Mtu kweli alianifuata akaniambia mimi nataka nisitiriwe na niolewe, nitafanyaje na yeye pia ndiye pia kasema nataka nitoke na katoka? Ni kweli. Kila kitu alitaka yeye," alisema.

Msizwa na Esma walifunga pingu za maisha mwaka wa 2020 ila pingu hizo zikawashikilia kwa kipindi kifupi tu kwani hatimaye waliachana baada ya miezi mitatu tu.

Msizwa ameweka wazi kuwa wake zake wengine walikuwa sawa kwa yeye kumuoa Esma kama mke wa tatu.

"Wake zangu niliwapa taarifa kuwa naoa na wakaridhia. Niliwaambia kuna mtu anataka nimsitiri wakasema sawa ataungana na wao na watakuwa tayari. Esma alikuwa mke wa tatu. Yeye ndiye aliniomba kufanya hivyo," alisema.

Mfanyibiashara huyo pia alidokeza kuwa Esma kisheria bado ni mke wake kwa sababu bado hawatalikiana.

Aidha alitupilia mbali madai kuwa alijitosa kwenye ndoa na dada huyo wa Diamond kwa ajili ya kujizolea umaarufu.

Takriban mwezi mmoja Bw Msizwa alijitenga mbali na madai kwamba alitumia uchawi kumtongoza Esma.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa hoteli yake, Bw Msizwa alidai kuwa dada huyo wa Diamond ndiye aliyemtongoza.

"Mimi ndiye nilitongozwa. Sio mimi nilienda kumtongoza yeye. Hiyo kabisa nakwambia. Aliniambia anataka nimuone ili nimsitiri,"  alisema.

Pia alitupilia mbali madai kuwa ndoa yake na Esma ilikuwa ni biashara tu na kusisitiza kuwa walikuwa wameoana kwa kweli.

"Tulioana kwa kweli lakini ikatokea sintofahamu ikawa hivo na huwezi kulazimisha kitu ambacho kimetokea," alisema.

Mfanyibishara huyo alisisitiza kwamba yeye sio sababu ya kutengana kwao. Alibainisha kuwa ana wake wengine wawili ambao wamekaa naye kwa miaka mingi tofauti na Esma ambaye alikaa kwa muda mfupi sana

"Mimi sipendi matatizo. Umri niliofikia sijawahi kukaribisha matatizo. Kama Mtu alikuja akaondoka yeye ndiye mwenye matatizo, sio mimi," alisema.

Msizwa na Esma walifunga ndoa mnamo Julai 30, 2020 ila wakatengana na kuenda njia tofauti miezi mitatu baadae.