Judy Nyawira afunguka jinsi alivyopata ujauzito wa Abel Mutua akiwa chuo kikuu

“Tulipima ikawa iko, nikalia nikalia. Nilikuwa nalala, nalia mpaka kichwa kinauma," Judy alisimulia.

Muhtasari

•Judy alifichua kwamba alikuwa katika mwaka wake wa tatu chuoni alipopata ujauzito wa mtoto wao wa pekee, Stephanie Mumbua.

•Judy alibainisha kuwa alichagua kuhifadhi ujauzito huo na aliendelea kuubeba akiwa bado anasoma hadi alipojifungua.

Judy Nyawira, Abel Mutua na Stephanie Mumbua

Judy Nyawira, mke wa muigizaji Abel Mutua amefunguka kuhusu jinsi alivyopata ujauzito wakati akiwa bado anasoma katika chuo cha Kenya Institute of Mass Communication (KIMC) zaidi ta mwongo mmoja uliopita.

Katika mahojiano na mtangazaji Oga Obinna, Judy alifichua kwamba alikuwa katika mwaka wake wa tatu chuoni alipopata ujauzito wa mtoto wao wa pekee, Stephanie Mumbua.

Alisema alianza kushuku kwamba alikuwa amebeba mtoto tumboni yapata wiki mbili baada ya kwenda nyumbani kwa likizo.

"Wiki moja kabla ya sisi kufunga shule, nilikuwa nimeanza kuhisi ajabu. Nilihisi mwili haukuwa kawaida. Nilianza kuhisi kuna kitu hapa. Maradhi ya asubuhi yalikuwa bado hayajaanza,” Judy alisimulia.

Aliendelea, “Wiki mbili baada ya kufika nyumbani nilianza kuhisi hapanaa. Niliona hapa kuna kitu, hapa lazima kuna kitu. Hakukuwa na maradhi ya asubuhi bado lakini nilikuwa tayari nimeanza kuhisi kuna kitu. Kwa hivyo tuliongea (na Abel) nikamwambia hapa vile naskia, kuna kamtu ndani ya tumbo hili. Wakati mwingine wanawake husema hawawezi kujua ni lini ni wajamzito lakini mimi nilihisi.”

Mama huyo wa binti mmoja alifichua kwamba wakati alipoanza kuwa na wasiwasi zaidi, tayari alikuwa na ujauzito wa wiki tano.

Wakati bado  akiwa nyumbani, alimpigia simu Abel na kumwarifu kuhusu wasiwasi wake kabla ya muigizaji huyo kumshauri amdanganye mama yake na kutafuta sababu ya kurudi Nairobi. Wakati huo, Abel alikuwa tayari amemaliza shule na tayari alikuwa akifanya kazi Tahidi High.

“Hakutaka nipime peke yangu, aliniambia niende tukapime pamoja. Nilimdanganya mama, mama akakubali na ndivyo nilijipata Nairobi na tulipima siku hiyo hiyo. Sikutaka kungoja, nilitaka tu nijue kama ni ukweli,” alisema Judy.

Alisema kipimo walichokifanya kilithibitisha hofu yake kwamba ni kweli alikuwa mjamzito, jambo ambalo lilimuathiri sana kisaikolojia.

“Tulipima ikawa iko, nikalia nikalia. Nilikuwa nalala, nalia mpaka kichwa kinauma, nalala tena naamka nikikumbuka naanza kulia tena. Abel alikuwa akinifariji tu. Mwisho wa siku tulifanya mazungumzo, ni mazungumzo ambayo tulihitaji kuwa nayo kuhusu kile ninachotaka kufanya na ujauzito,” alisimulia.

Alibainisha kuwa alichagua kuhifadhi ujauzito huo na aliendelea kuubeba akiwa bado anasoma hadi alipojifungua wakati akifanyia kazi mradi wake wa shule.

Judy alifichua kuwa alirudi shuleni kumalizia mradi wake wiki mbili tu baada ya kujifungua na angemwacha mtoto wake na shemeji yake ambaye alikuwa ameenda kukaa nao wakati ili kumpa nafasi ya kumaliza mradi wake wa shule.