Kajala acheka kitendo cha Harmonize kufuta tattoo yake na Paula

Kajala alionyesha waziwazi kwamba hasumbuliwi hata kidogo na hatua hiyo.

Muhtasari

•Kajala  ameonekana kujibu baada ya mpenzi wake wa zamani, Harmonize, kufuta tattoo yake na bintiye Paula Paul.

•Kajala alichapisha video fupi ya mvulana mdogo akijifanya kulia kisha ghafla anaanza kucheka

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Kajala
Image: HISANI

Aliyekuwa mpenzi wa Harmonize, Frida Kajala Masanja ameonekana kujibu baada ya mwimbaji huyo kufuta tattoo yake na bintiye Paula Paul.

Ilifichuka kuwa Harmonize amefuta tattoo hiyo ambayo amekuwa akibeba kwenye mguu wake kwa karibu mwaka mzima baada ya kuchapisha video yake akiimba na kucheza wimbo wake mpya, ‘Single Again’ siku ya Jumatano.

Katika video hiyo ambayo aliipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, ilifichua kuwa tattoo hiyo  imefunikwa. Harmonize hata hivyo hakueleza sababu yake ama wakati ambao alichukua hatua hiyo kubwa.

"Sijawahi kupenda wimbo wangu wowote kama ninavyoupenda wimbo huu," aliandika chini ya video hiyo.

Katika kile kilichoonekana kama jibu lisilo la moja kwa moja kwa mpenzi huyo wake wa zamani, Kajala alionyesha waziwazi kwamba hasumbuliwi hata kidogo na hatua hiyo.

Kwenye instastori zake, Kajala alichapisha video fupi ya mvulana mdogo akijifanya kulia kisha ghafla anaanza kucheka. Mama huyo wa binti mmoja hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu posti yake. Video hiyo inaonekana kuonyesha wazi kuwa hata hakukasirishwa na hatua ya mwanamuziki huyo.

Harmonize alipiga hatua ya kuchorwa tattoo ya picha ya kumbukumbu ya muigizaji huyo akiwa na binti yake Paula kwenye mguu wake mapema mwaka jana, wakati akiomba msamaha na kumsihi warudiane. Alitumia hiyo kama mojawapo ya njia ya kumtongoza ili warudiane baada ya kuwa wamekosana kwa mwaka.

Licha ya mahusiano yao kugonga ukuta mapema mwezi Desemba, mwimbaji huyo aliendelea kubeba tattoo hiyo kwenye mguu wake kwa zaidi ya miezi miwili kabla ya hatimaye kuchukua hatua ya kuifuta.

Mapema mwezi huu wakati alipofanya ziara ya muziki nchini Kenya, Harmonize alijibu kwa nini bado hakuwa ameifuta.

"Tatoo ni suala la kibinafsi. Sidhani kama ni kitu unaweza kuzungumza kuhusu.Tuangalie tu kama itakuwepo," alisema.

Wakati wa mahusiano yao, Harmonize na Kajala pia walichorwa tattoo za herufi ya kwanza ya majina yao kwenye vidole. Bado haijabainika wazi kama kwamba amefuta tattoo hiyo nyingine pia.