Kajala afichua kwa nini anampenda mchumba wake Harmonize

Kajala alibainisha kuwa mwimbaji huyo huwa hakati tamaa anapotaka kitu.

Muhtasari

•Kajala alimpongeza mchumba wake na kumhakikishia usaidizi wake katika kila kitu anachokusudia kufanya.

•Aliongeza,  "Endelea, ninakuunga mkono hommie @harmonize_tz."

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Muigizaji wa Bongo Fridah Kajala Masanja amefunguka kuwa anavutiwa sana na dhamira kubwa ya mchumba wake Harmonize.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram, Kajala alibainisha kuwa mwimbaji huyo huwa hakati tamaa anapotaka kitu.

Mama huyo wa binti mmoja alimpongeza mchumba wake na kumhakikishia usaidizi wake katika kila kitu anachokusudia kufanya.

“Kitu kimoja ninachokipenda kwako ni kuwa unapotaka kitu, hukati tamaa mpaka ukipate. Ndio maana nakupenda,” alisema. 

Aliongeza,  "Endelea, ninakuunga mkono hommie @harmonize_tz."

Kajala aliambatanisha ujumbe huo na picha nzuri inayomuonyesha akifurahia wakati mzuri na mchumba huyo wake.

Juhudi za Harmonize za kurudiana na Kajala mapema mwaka huu ni uthibitisho kwamba huwa hakati tamaa. Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alifaulu kumshawishi muigizaji huyo kurudiana naye baada ya takriban miezi miwili ya kuomba msamaha.

Hivi majuzi, Harmonize alifichua kuwa wimbo wa sita katika albamu yake mpya  'Made For Us',  'Utanikumbuka' ulihamasishwa na mchumba wake Kajala ambaye pia ni meneja wake. Alisema mapambano aliyopitia kumshawishi muigizaji huyo amsamehe hadi akubali kurudiana naye yalimfanya afanye wimbo huo.

"Nilitengeneza wimbo huo wakati wa kipindi cha 'nikubali tena'. Nilimbembeleza sana!! Nilifanya kila kitu kumuonyesha kiasi gani najutia na kiasi gani namhitaji tena," alisema baada ya kuzindua albamu hiyo.

Mwimbaji huyo alifichua kuwa haikuwa rahisi kumshawishi mama huyo wa binti mmoja kuhusu nia yake naye kwa kuwa hata watu waliokuwa wamemzunguka wakati huo walikuwa wakimshauri dhidi yake wakidai alikuwa akitafuta kiki tu.

"Sasa tuko hapa na masiku yanayoyoma!! Mwaka unaelekea kukatika usichoke, usikatize tamaa, ndoto zako akikuelewa Mungu peke yake inatosha. Binadamu watakuelewa mbele ya safari!! " alisema.

Alisema aliifanya albamu hiyo akiwaza jinsi mchumba wake ambaye walikuwa wameachana naye wakati huo angemkumbuka.

Staa huyo alitumia zaidi ya miezi miwili, mamilioni ya pesa na akalazimika kustahimili kejeli nyingi mitandaoni wakati akijaribu kumshawishi Kajala akubali kurudiana naye tena.

Hatimaye ombi lake la msamaha lilifaulu na wakarudiana mwezi Mei. Kwa sasa wawili hao wanatazamia kufunga pingu za maisha kwani Harmonize tayari amemvisha mchumba huyo wake pete ya uchumba.