Kakake Baha na mpenziwe watengana mwaka mmoja baada ya kupoteza mtoto wao

Mungai na Aisha walimpoteza mtoto wao mwezi mmoja tu baada ya kuzaliwa.

Muhtasari

•Mungai Mbaya ametangaza kuwa mahusiano yake na mwanamitindo huyo yaligonga ukuta hivi majuzi.

•Mnamo Juni 28, 2021  Mungai na Aisha walimpoteza mtoto wao Lyric Kagecho Mungai, mwezi mmoja tu baada ya kuzaliwa.

Mungai Mbaya na Aisha Mohammed
Image: MAKTABA

Muigizaji wa zamani wa Machachari, Mungai Mbaya ametangaza kutengana kwake na mpenziwe Aisha Mohammed.

Mungai ametangaza kuwa mahusiano yake na mwanamitindo huyo yaligonga ukuta hivi majuzi baada ya kuchumbiana kwa muda mrefu.

Alidokeza kuwa alitengana na Bi Aisha baada ya mambo katika uhusiano wao kukosa kukidhi  matarajio yao. Mungai hata hivyo alibainisha kuwa hakuna uhusiano mbaya kati yao licha ya kutengana.

"Mimi na Shorty tuliachana hivi majuzi. Huenda baadhi yenu mmetambua. Nilichagua kulizungumzia kwa sababu ninachoshwa na maswali yote kwenye Dms. Hata hivyo tuko sawa, sina lingine  ila upendo kwake, nina uhakika anahisi vivyo hivyo. Mambo yalikuwa tofauti na tulivyotarajia. Daima tutakuwa baba na Mama Lyric," Mungai alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kaka huyo wa muigizaji Tyler Mbaya almaarufu Baha pia aliwashukuru mashabiki wake kwa upendo mkubwa ambao  walimuonyesha pamoja na mpenziwe katika kipindi kigumu ambacho walipitia mwaka jana.

Mnamo Juni 28, 2021  Mungai na Aisha walimpoteza mtoto wao Lyric Kagecho Mungai, mwezi mmoja tu baada ya kuzaliwa.

Bi Aisha alimuomboleza mwanawe ambaye alizaliwa Mei 28, 2021 na kudokeza kuwa alifariki baada ya kushindwa kustahimili maumivu aliyokuwa nayo.

"Yeye ndiye mtoto mzuri zaidi ambaye nimewahi kuona. Alikuwa mtoto mwenye furaha na amani na ninafurahi sana kukutana naye na kumfahamu kwa mwezi huo mmoja. Alitimiza mwezi mmoja leo lakini hakuweza kuendelea zaidi. Nilikuwa na mipango mingi kwa ajili yake na inauma sana kwamba sitawahi kuonana naye. Siamini mwanangu ameondoka😭😭😭Yaani bado niko kwenye mshtuko na kukataa.'' Aisha alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram mnamo Juni 28, 2021.

Aisha na Mungai wamekuwa wakimkumbuka mtoto huyo wao mara kwa mara na kuchapisha jumbe za kihisia kwenye mitandao ya kijamii.

Kutengana kwa wapenzi hao wa muda mrefu kumejiri  takriban mwaka mmoja tu  baada ya kumpoteza mtoto wao.