Kanye West amshtumu aliyekuwa mkewe kwa kutoka kimapenzi na mwanaspoti maarufu

Rapa huyo amedai kwamba matumizi ya video na picha chafu ilisambaratisha familia yake.

Muhtasari

•Kanye West na Kim Kardashian watashiriki malezi ya pamoja ya watoto wao wanne baada ya talaka yao kusuluhishwa.

•Rapa huyo amedai kuwa aliwahi kumfumania mkewe na mchezaji wa mpira wa vikapu Chris Paul

Kim Kardashian na aliyekuwa mume wake Kanye West
Image: HISANI

Rapa wa Marekani Kanye West almaarufu 'YE' amemshtumu mke wake wa zamani Kim Kardashian kwa kutokuwa mwaminifu wakati wa ndoa yao iliyosambaratika.

Kim Kardashian aliwasilisha rasmi maombi ya talaka na Kanye West mnamo Februari 19, 2021 akitaja tofauti zisizoweza kusuluhishwa.Wanandoa hao wa zamani ambao walikuwa pamoja kwa takriban miaka sita sasa watashiriki malezi ya pamoja ya watoto wao wanne baada ya mahakama kusuluhisha talaka yao mapema wiki hii.

Kanye West sasa ameibua madai kwamba mzazi huyo mwenzake aliwahi kutoka kimapenzi na mchezaji wa mpira wa kikapu wa Marekani, Chris Paul.  Kupitia ukurasa wake wa Twitter, West amedai kuwa aliwahi kumfumania mkewe na Paul.

“Hebu tuvunje dirisha la mwisho kabla hatujatoka hapa, nilimpata huyu jamaa akiwa na Kim, Usiku mwema," rapa huyo alisema Ijumaa asubuhi na kuambatanisha ujumbe wake na picha ya mwanaspoti huyo mwenye umri wa miaka 37.

Katika chapisho lingine, mwanamuziki huyo bwenyenye alidai kwamba matumizi ya video na picha chafu ilisambaratisha familia yake.

"Matumizi ya picha chafu yaliharibu familia yangu lakini Yesu atatengeneza kila kitu," alisema.

Muda mfupi baada ya kuibua madai hayo mazito, akaunti ya Twitter ya Kanye West ilifungwa kwa mara nyingine.

Bosi wa Twitter Elon Musk ameeleza kuwa akaunti hiyo ilisimamishwa kwa madai ya uchochezi wa vurugu.

"Kufafanua tu kwamba akaunti yake imesimamishwa kwa uchochezi wa vurugu, sio picha isiyopendeza ya mimi na Ari. Kwa kweli, nilipata picha hizo kuwa motisha ya kusaidia kupunguza uzito!," alisema.

Siku chache zilizopita, Kanye West aliagizwa kumlipa Kim Kardashian $200,000 (Ksh 24.5M) kwa mwezi kama matunzo ya watoto katika makubaliano ya talaka.

Rapa huyo wa zamani na nyota wa televisheni atashiriki malezi ya pamoja ya watoto wao wanne.

Hii inakuja wiki chache tu baada ya kampuni kadhaa kukata uhusiano na Ye juu ya maoni ya chuki.

Masuala kuhusu mgawanyo wa mali na malezi ya watoto wao yalitatuliwa katika hati za mahakama zilizowasilishwa Jumanne.

Pande hizo mbili zinapaswa kushauriana na kila mmoja juu ya maamuzi makuu kuhusu ustawi wa watoto wao, nyaraka zinasema.

Gharama za usalama wa watoto, shule na chuo zitagawanywa.

Kwa kuongeza, Ye anatarajiwa kulipa $200,000 kwa mwezi kama msaada wa watoto - ambayo New York Post iliripoti ni kwa sababu watoto watatumia muda wao mwingi na Kardashian.

Wanandoa hao wana watoto wanne.