"Kuolewa kunapararisha!" Amira asuta ndoa yake na Jamal huku wakirushiana vijembe

Jamal na Amira wameendelea kutupiana vijembe miezi kadhaa baada ya kutengana.

Muhtasari

•Katika chapisho lake Amira alikuwa amedokeza kwamba "Ukianza kujizingatia mwenyewe maisha yako yanaenda juu."

•Jimal aliwashauri wafuasi wake kutafuta wapenzi wenye kusamehe iwapo wanakusudia kufunga ndoa.

Amira na aliyekuwa mumewe, Jamal Rohosafi
Image: INSTAGRAM

Wanandoa wa zamani Jimal Marlow Rohosafi na Amira wameendelea kutupiana vijembe mitandaoni miezi kadhaa baada ya kutengana.

Ndoa ya wawili hao ya muda mrefu ilisambaratika mwishoni mwa mwaka jana baada ya Jimal kuonekana kumchagua aliyekuwa mkewe wa pili, mwanasoshalaiti Amber Ray, badala ya mkewe wa kwanza.

Baadhi ya wanamitandao wamekuwa makini kugundua kuwa Amira amekuwa aking'aa zaidi tangu alipogura ndoa yake.

"@being_amira Tangu uwachane na Jamal walahi umekuwa mrembo zaidi na unang'aa. Unakaa mzungu," mtumizi mmoja wa Instagram alitoa maoni chini ya chapisho moja la mama huyo wa wavulana wawili

Katika chapisho lake Amira alikuwa amedokeza kwamba "Ukianza kujizingatia mwenyewe maisha yako yanaenda juu."

Huku akimjibu mwanamitandao huyo, mfanyabiashara huyo alikosoa ndoa akitaja kuwa inawafanya watu kuparara.

"Kuolewa kunapararisha😂.." alijibu.

Shabiki mwingine alimpongeza kwa kufanikiwa kumfundisha somo mzazi mwenzake kwa matendo yake ya awali.

"Walahi Jamal amejichuna masikio🤣🤣. Na liwe funzo kwa wengine wenye tabia kama yake! Mwanamke akiamua, imeisha," mtumizi mwingine wa Instagram alimwambia Amira.

Alijibu kwa kusema, "akule kachumbari zake pole pole."

Siku ya Jumamosi Jimal aliwashauri wafuasi wake kutafuta wapenzi wenye kusamehe iwapo wanakusudia kufunga ndoa.

Katika chapisho lake la Instagram, mwenyekiti huyo wa muungano wa wamiliki matatu jijini Nairobi alionekana kumchana Amira.

"Wakati Unachumbiana Ili Kuoa, chumbiana na mpenzi mwenye kusamehe, Sio yule ambaye ataleta Masuala Kutoka Nazareti Hadi Galilaya 🤣," alisema.

Mwezi Julai Jimal alikiri majuto yake kwa kusababisha kuvunjika kwa ndoa yake na kuomba msamaha kutoka kwa Amira.

Mfanyibiashara huyo  alikiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao.

"Naomba radhi kwa kukukosea heshima, kukuaibisha, kwa kukuumiza, kwa maumivu yote na kwa huzuni niliyokuletea. 💔Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," alisema.

Pia alikiri kuwa alikosa kutimiza  wajibu wake wa kumlinda mkewe kama alivyohitajika kufanya. Alisema kwamba alifahamu wakati ndoa yake ikiporomoka ila akashindwa na la kufanya kwa wakati ule.

"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.

Jamal pia alikiri kwamba hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake na mama ya watoto wake.

Katika jibu lake kwa ombi hilo la msamaha Amira hata hivyo alidokeza kuwa anahitaji muda kwani "vidonda vingine haviponi."