Maajabu! Kumbe Zari alianza kuchumbiana na Shakib punde baada ya kutengana na Diamond

Taarifa mpya zimeibuka kuwa Shakib amekuwa akichumbiana na Zari kwa takriban miaka 4.

Muhtasari

•Shakib mwenyewe, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Tiktok alifichua kuwa wamekuwa wakisukuma mapenzi yao kwa miaka kadhaa.

•Ikiwa maelezo yanayojitokeza ni ya kweli, basi inamaanisha  Zari alikutana na mpenziwe huyo mara baada ya kutengana na Diamond.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Penzi la mwanasoshalaiti maarufu Zari Hassan na mpenzi wake mdogo Shakib Cham Lutaaya limeendelea kunoga kadri siku zinavyosonga.

Mahusiano kati ya wapenzi hao  wawili yalikuja kujulikana takriban miezi minne iliyopita, miezi michache tu baada ya Zari kutengana na mfanyibiashara wa Uganda GK Choppa.

Cha kushangaza sasa ni kwamba, taarifa mpya zimeibuka kuwa Shakib amekuwa akichumbiana na mwanasoshoalaiti huyo kutoka Uganda kwa takriba miaka minne. Shakib mwenyewe, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Tiktok alifichua kuwa wamekuwa wakisukuma mapenzi yao kwa miaka kadhaa.

"Miaka minne pamoja..🥂❤ #Wanandoa #Hadithiyamapenzi," alisema chini ya video ya kumbukumbu zao pamoja.

Katika video hiyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana akiwa amemshika Zari walipokuwa wakiingia ndani ya klabu.

Ikiwa maelezo yanayojitokeza ni ya kweli, basi inamaanisha  Zari alikutana na mpenziwe huyo mara baada ya kutengana na Diamond.

Zari na Diamond walikuwa wameishi pamoja kama wanandoa kwa miaka minne kabla ya kuachana mnamo siku ya wapendanao 2018. Baada ya kutengana na staa huyo wa Bongo, Zari hata hivyo amewahi kuonekana na mwanaume mwingine hata kabla ya mahusiano yake na Shakib kuja kujulikana hatimaye.

Inaaminika kuwa mwanasoshalaiti huyo alikuwa kwenye mahusiano na GK Choppa kwa miezi kadhaa kabla ya kutengana katika hali tatanishi. Wakati wa mahusiano yao, Zari alipakia picha zake na Mganda huyo mara kwa mara.

Mwezi uliopita Zari Hassan alidokeza kufunga pingu za maisha na Bw Shakib Cham Lutaaya baada ya kufichua kuwa mpenzi huyo wake wa sasa anapanga kupeleka posa kwa baba yake nchini Uganda.

"Shakib aliniambia jana kuwa anataka kukutana na baba yangu. Anataka kutoa posa kwa ajili ya ndoa, yuko tayari kunioa," Zari alisema kwa Kiganda  katika video ambayo ilipakiwa kwenye mtandao wa Snapchat.

Katika video hiyo fupi, mama huyo wa watoto watano aliendelea kuwatupia vijembe wakosoaji wa mahusiano yake na Bw Shakib huku akiwathibitishia kuwa juhudi zao kuwatenganisha zilikuwa zimefeli.

"Waliosema itaishia kwa machozi rudini kwa waganga wenu mkaombe warudishe hela, uchawi haukufanya kazi," alisema.

Hapo awali  mwanasoshalaiti huyo alikuwa amebainisha kuwa mpenzi wake mpya amemletea amani ambayo imemwezesha kukua na kung'aa zaidi.

"Nanza kuwa mkubwa. Naona shavu. Nimejipa amani sana. Bwana Lutaaya unanipa amani sana  kwa maana, watu, ngojeni niwaambie kuhusu amani ya  akili, hiyo nawaambia hata ufanye nini, unakua mkubwa zaidi hata usipokula," alisema kupitia Tiktok.

Mwanasoshalaiti huyo alimtaka Shakib kuendelea kumpatia mahaba anayompa na kumbainishia kuwa yanafanya kazi.

"Bwana Lutaaya chochote unachofanya, ongeza zaidi. Niongezee dozi nyingine, chochote unachofanya kwa sababu zinafanya kazi, zinafanya kazi. Hata hao wanaoroga wamekata tamaa, wanahitaji kurejeshewa pesa zao. Bado nina amani, nendeni mkaombe kurejeshewe pesa zenu," alisema.

Zari amekuwa akitetea mahusiano yake na Lutaaya hasa kwa kuwa amekosolewa sana kufuatia utofauti wao wa kiumri.