Mahaba Ndi Ndi Ndi! Kajala hatimaye amjibu Harmonize kwa mara ya kwanza tangu kutengana kwao

Muhtasari

•Kajala hatimaye amejibu chapisho moja la Harmonize kwenye Instagram kwa mara ya kwanza tangu walipokosana.

•Harmonize alisema anaumizwa sana na kejeli ambazo amekuwa akipokea kutokana na juhudi zake za kuomba msamaha

Harmonize na Kajala Masanja
Harmonize na Kajala Masanja
Image: HISANI

Huenda Kajala Masanja hatimaye amekubali msamaha wa Harmonize na hata kurudiana naye tayari kulingana na matukio ya hivi majuzi.

Muigizaji huyo hatimaye amejibu chapisho moja la Harmonize kwenye Instagram kwa mara ya kwanza tangu walipokosana zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Harmonize alichapisha ujumbe mrefu akimshukuru muigizaji huyo kwa kusimama naye katika hali zote licha ya mabaya aliyomtendea.

"Wakati Dunia Nzima inasema Haiwezekani Ulisimama Ukasema Inawezekana. Ulinipenda nami mbaya zaidi Ulikutana na Disappointment  ambayo iliwapa nguvu na ujasiri kila mtu aliye karibu yako kusema mimi sio binadamu wa kuwa hata karibu yako. Najua uliumia sana ...!!!! Bado hukunikatia tamaa. Wakati Mwingine binadamu huingia kwenye mahusiano ukiamini kwamba unaweza kumsahau yule uliyekuwa naye mwanzo bila kuwaza niini kiliwafanya muwe pamoja. Nilipitia hicho kipindi na picha zikamwagika mtandaoni na nikajiona nimemaliza wala sikujali maumivu yako. Bado ulikaa kimya, hakuna mahojiano licha ya kuahidiwa marundo ya pesa ambayo ungeweza kununua hata hivyo vigari wanavyoviona ni kitu cha maana sana,"  Harmonize aliandika chini ya picha ya Kajala ambayo alipakia Instagram Jumapili.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliweka wazi kuwa tayari anayajuta mabaya yote ambayo alimtendea Kajala pamoja na familia yake.

Alisema tattoo ya muigizaji huyo na binti yake ambayo alichorwa kwenye mguu wake ni ishara ya majuto na ombi la msamaha kwake litakalosalia pale daima.

"Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa nilikosea familia yangu. Hakuna ambacho kitabadilisha kuwa ni familia yangu. Pia hakuna ambacho kitabadilisha kuwa najivunia familia yangu Mguu Wangu wa kulia utasema Sorry mpaka Siku Yangu Ya Mwisho," Alisema.

Mwanamuziki huyo alisema anaumizwa sana na kejeli ambazo amekuwa akipokea kutokana na juhudi zake za kuomba msamaha. Alisema kuwa anajaribu kuwa mume bora kwa Kajala.

"Nakupenda sana mke wangu Frida Kajala," Alisema.

Ni wazi kuwa ujumbe huo mrefu ulimfikia mlengwa kwani chini yake Kajala alijibu kwa emoji zinazoashiria pongezi na upendo.

"🙏🏽🙏🏽🙏🏽❤️" Kajala alijibu.

Jibu la Kajala liliwasisimua mashabiki wengi wa Harmonize ambao walijumuika pale na kuacha jumbe nzuri za kheri.