Mambo ni kortini sasa! Mulamwah kumshtaki Carrol Sonie, aibua madai mazito dhidi yake

Mulamwah alibainisha amefanya uamuzi wa kuelekea mahakamani baada ya juhudi za kutatua masuala yao kidiplomasia kushindwa.

Muhtasari

•Mulamwah ametishia kumshtaki mzazi mwenzake Caroline Muthoni Ng’ethe huku drama kati ya wapenzi hao wawili wa zamani ikiendelea.

•Mulamwah alamika kuhusu video ya hivi majuzi ambayo Sonie ambapo inadaiwa alimsingizia kuwa amepuuza majukumu yake ya malezi ya mtoto. 

Mulamwah na Carrol Sonnie
Image: INSTAGRAM/CAROL SONNIE

Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah ametishia kumshtaki mzazi mwenzake Caroline Muthoni Ng’ethe huku drama kati ya wapenzi hao wawili wa zamani ikiendelea.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, baba huyo wa binti mmoja alibainisha kuwa amefanya uamuzi wa kuchukua hatua za kisheria baada ya juhudi za kutatua masuala yao kwa njia ya kidiplomasia kushindwa.

Mulamwaha alishiriki barua ndefu iliyoandikwa na mawakili wake kwa mpenzi huyo wake wa zamani akieleza kutoridhika kwake na jinsi Sonie amedaiwa kupuuza barua ya awali na jinsi ambavyo amedaiwa kuendelea kuibua madai ya uwongo dhidi yake.

"Umeendelea kumchafulia jina mteja wetu bila sababu huku ukimnyima haki ya kumuona mtoto," barua hiyo iliyotiwa saini na MNO Advocates LLP ilisoma.

Katika barua hiyo, Mulamwah aliendelea kulalamika kuhusu video ya hivi majuzi ambayo mpenzi huyo wake wa zamani aliifanya kwenye YouTube ambapo inadaiwa alimsingizia kuwa amepuuza majukumu yake ya malezi ya mtoto. 

"Ulizua maoni ya uwongo kwamba mteja wetu amekataa na/au amepuuza kushiriki gharama ya kumlea mtoto. Hii ni licha ya kukiri kwako kwamba mara kadhaa mteja wetu amekutumia pesa kupitia MPESA kwa ajili ya matunzo ambayo umeghairi bila kutoa sababu,” barua hiyo ilisoma.

Mchekeshaji huyo pia alilalamika kuhusu muigizaji huyo kuondoa jina lake kwenye cheti cha kuzaliwa cha binti yao.

Aidha, alitumia fursa hiyo kutangaza nia yake ya kumshirikisha mpenzi huyo wake wa zamani katika majadiliano yanayohusiana na malezi ya msichana wao wa miaka miwili.

Kufuatia malalamiko yote aliyotoa, Mulamwah aliendelea kutoa madai matatu makuu kwa mama huyo wa bintiye.

Madai hayo ni pamoja na;

i) Kufuta taarifa za kumchafulia jina na kuomba msamaha hadharani.

ii) Kufuta picha na video zote za mtoto kwenye chaneli yake ya YouTube.

iii) Kushiriki stakabadhi ya cheti cha sasa cha kuzaliwa cha mtoto wao na sababu ya kubadilisha jina lake bila ridhaa yake.

"Tafadhali kumbuka kuwa mteja wetu yuko tayari kukupa siku 10 kuanzia tarehe ya kupokea barua hii ili kutii kama ilivyoelezwa hapo juu," ilisoma taarifa iliyoandikwa Februari 1, 2024.