"Mapenzi ni kamari!" Harmonize amtambulisha mpenziwe mpya mwezi tu baada ya kumtema Kajala

Harmonize amezama kwenye dimbwi la mahaba na mwimbaji mwenzake Feza Kessy.

Muhtasari

•Siku ya Alhamisi asubuhi, Harmonize alidokeza kwamba amezama kwenye dimbwi la mahaba na mwimbaji mwenzake Feza Kessy.

•Wawili hao walionekana kustarehe na wenye furaha kubwa kwa kuwa pamoja.

Harmonize na anayedaiwa kuwa mpenzi wake mpya Feza Kessy
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarafu Harmonize amedokeza mahusiano mapya takriban mwezi moja tu baada ya kutengana na muigizaji Fridah Kajala Masanja.

Siku ya Alhamisi asubuhi, Harmonize alidokeza kwamba amezama kwenye dimbwi la mahaba na mwimbaji mwenzake Feza Kessy.

Bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alichapisha picha kadhaa zinazomuonyesha akiwa na kipusa huyo kwenye bahari na kuambatanisha na ujumbe uliofichwa ukidokeza kwamba wawili hao wanachumbiana.

"No mara waaa!!! @fezakessy ❤❤," aliandika chini ya picha hizo ambazo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Harmonize pia alichapisha video yao fupi kwenye Instastori ambayo inawaonyesha wakifurahia muda pamoja  ndani ya nyumba, wawili hao walionekana kustarehe na wenye furaha kubwa kwa kuwa pamoja.

Katika video hiyo, Feza ambaye alikuwa amevalia nguo nyepesi ya kulala alionekana akiwa amestarehe kwenye kiti huku Harmonize ambaye alionekana amevalia kaptura nyeusi pekee akitengeneza kucha zake.

"Mapenzi ni kamari," aliandika chini ya video hiyo.

Mashabiki wengi wa wasanii hao wamehitimisha kuwa wapo kwenye mahusiano na tayari wamechukua hatua ya kuwapongeza.

Muigizaji Kajala Masanja alitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana baada ya wawili hao kuchumbiana kwa miezi michache. Walikuwa wamerudiana mwezi Mei 2022 baada ya Harmonize kuomba msamaha.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema kupitia Instagram.

"Hakika nimekosea familia yangu, ndugu zangu, na marafiki zangu. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa. Namsemehe X wangu na niko tayari kuenda kwa mwingine." 

Harmonize hata hivyo amesalia kimya kuhusu kutengana na Kajala Masanja licha ya shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wake  wakimtaka aweke wazi yaliyojiri kati yake na muigizaji huyo mkongwe wa Bongo.