Meneja wa Diamond, Babu Tale afunguka suala la kuoa tena baada ya kufiwa na mkewe

Tale alisema angependa kupata mwanamke anayelingana na sifa za marehemu mkewe.

Muhtasari

•Shammy alikata roho mnamo Juni 28, 2020 na habari za kifo chake kutangazwa kwanza na  Mama Dangote.

•Tale ameeleza kuwa kwa muda mrefu amekuwa akipiga sala kumuomba  Mungu amtunuku na mke mwingine mwema.

Meneja wa Wasafi, Hamisi Taletale almaarufu Babu Tale amekiri kuwa bado hajaweza kusonga mbele kimahusiano kufuatia kifo cha mkewe.

Ni takriban miaka miwili ambayo imepita sasa tangu Babu Tale alipompoteza mke wake , Bi Shammy Tale.

Shammy alikata roho mnamo Juni 28, 2020 na habari za kifo chake kutangazwa kwanza na  Mama Dangote.

"Mke na mama watoto wa meneja wa lebo ya WCB Hamis Taletale, Shammy alifariki mapema hii leo," Mamake Diamond alitangaza kupitia mitandao ya kijamii.

Marehemu aliwaacha nyuma watoto wanne ambao Babu Tale amekuwa akiwalea pekee yake kwa kujivunia.

Babu Tale akizungumza na waandishi wa habari ameweka wazi kuwa bado anaendelea kuponya majeraha ya kufiwa na mkewe na kubainisha kuwa bado hajapata wa kujaza pengo kubwa ambalo marehemu Shammy aliacha.

"Mi bado sijamove on. Nadhubutu kusema hivo. Lakini nimemwachia Mwenyezi Mungu atanitafutia zawadi nyingine. Amechukua zawadi, amenipa zawadi ya ubunge na akanipa zawadi ya mke mwema," Alisema.

Tale ambaye pia ni mbunge wa Morogoro Kusini alidokeza kuwa angependa kupata mwanamke anayelingana na sifa za marehemu mkewe.

Pia alieleza kuwa kwa muda mrefu amekuwa akipiga sala kumuomba  Mungu amtunuku na mke mwingine mwema.

"Bado niko nalia na Mungu. Ndio maana muda wote nipo kwenye ibada nikimuomba Mwenyezi Mungu anipe Shamsha mwingine," 

Mwaka jana meneja huyo wa WCB alifichua kwamba marehemu mkewe alimuachia ombi kuwa asioe tena.

"Mke wangu aliniambia nisioe tena. Nakumbuka siku hiyo nikiwa naye hospitalini, Aliniambia alikuwa amechoka kuwa mgonjwa na akanishika mkono na kuniambia, 'Ninaondoka, tunza watoto na usioe tena.'" Tale alisema kupitia Instagram.

Kipindi hicho Tale pia alipuuzilia mbali madai ya wanamitandao kuwa alikuwa na mpango wa kuoa tena.