Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili Ringtone Apoko na mwanasiasa Casypool walihusika katika ugomvi katika eneo la Kahawa West, kaunti ya Nairobi siku yaJumanne jioni.
Video iliyoshirikiwa na 2mbili ilimuonyesha mwimbaji huyo wa kibao ‘Pamela’ akishuka kutoka kwenye gari lake na kwa hasira akaelekea kumshambulia Casypool wakati alipokuwa akishirikigumzo na mchekeshjaji huyo.
Katika video hiyo, Ringtone alionekana akivua shati lake na kukunja ngumi ili kumpiga mwanasiasa huyo huku akimshutumu kwa kuharibu jina lake.
“Mimi ni yatima, wewe unaniharibia jina. Mimi naishi Wanyee?? Mimi ni yatima, huwezi kuniharibia jina? Mimi naishi Wanyee??,” Ringtone alisikika akimfokea Casypool huku mchekeshaji YY akijaribu kuwatenganisha.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alimshutumu Casypool kwa kueneza uvumi kwamba amewekwa na mwanamke mzungu.
Katika utetezi wake, Ringtone alikanusha madai hayo na kuweka wazi kuwa yeye binafsi ameng’ang’ana hadi kuweza kufadhili maisha yake ya kifahari katika mtaa wa Runda.
“Kwa nini mtu anashinda akisema naishi Wanyee? Eti kuna mzungu ameniweka? Mzungu ameniweka amenipea mzungu? Mimi ni yatima nimeng’ang’ana kuishi Runda. Sawa,” Ringtone alisema kabla ya kurudi kwenye gari lake.
“Aniheshimu mimi ni mwenyekiti. Mimi nimeokoka lakini kuna wakati Yesu alisema mapepo ingine inapigwa,” aliongeza.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili aliyezingirwa na utata katika maisha yake aliendelea kumtaka Casypool amheshimu na kuepuka kuchafua jina lake.
Casypool hata hivyo alionekana kukosa radhi na kudai kuwa angempiga mwimbaji huyo vibaya.
“Hawezi kunifanya kitu. Yeye hawezi kunitisha bana. Aende atye watu wengine bana. Huyo ni mtoto mdogo. Nimemlima huyo. Ningemuua huyo mtoto mdogo,” alisema.
Baada ya hayo Ringtone aliondoka tu huku mpinzani wake akiendelea kutulizwa na YY, 2mbili na watu wengine waliokuwa naye.