"Mimi sio shabiki wake!" Zari azungumza baada ya kukosa kukutana na Diamond nchini Kenya

Muhtasari

•Zari amefichua kuwa kuna mengi ambayo hufanyika kati yake na mpenzi huyo wake wa zamani bila ya wao kutangaza.

•Zari alikiri kuwa ni kweli hakukutana na baba huyo wa watoto wake wawili ila akaeleza kuwa walizungumza kwa simu.

Zari Hassan na Diamond Platnumz
Zari Hassan na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// TIFFAH DANGOTE

Mwanasoshalaiti maarufu  Zari Hassan ameweka wazi kwamba huwa anawasiliana na  Diamond Platnumz mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua Tanzania kwa ziara ya kikazi, Zari alifichua kuwa kuna mengi ambayo hufanyika kati yake na mpenzi huyo wake wa zamani bila ya wao kutangaza.

Alieleza kuwa yeye na Diamond hujadialiana kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu ikiwamo namna ya kulea watoto wao wawili pamoja.

"Mimi kuonana na Diamond ama familia yake sio lazima iwe kwenye vyombo vya habari. Tumeshakuwa familia. Mimi naongea na Diamond kila wakati kuhusu watoto na jinsi ya kuwalea. Sio lazima nikikutana naye nipost, mimi sio shabiki  wake, mimi ni mama ya watoto wake,"" Zari alisema.

Mama huyo wa watoto watano alikuwa anajibu madai kuwa hakupata nafasi ya kukutana na Diamond wakati wote wawili walipokuwa nchini Kenya siku chache zilizopita.

Zari alikiri kuwa ni kweli hakukutana na baba huyo wa watoto wake wawili ila akaeleza kuwa walizungumza kwa simu.

"Hatukukutana lakini tuliongea. Ni wazi tuliongea huku akiniambia kuwa yupo pale nami nikamwambia nipo kwa ajili ya kazi," Alisema.

Takriban wiki mbili zilizopita wazazi wenza hao wawili kutoka mataifa jirani walizuru Kenya kwa sababu tofauti. 

Zari ambaye ndiye aliyewasili wa kwanza alikuwa kwenye ziara ya kikazi huku Diamond akisalia kimya  kuhusu madhumuni ya ziara yake.

Licha ya kuwa wawili hao walitengana miaka kadhaa iliyopita, Zari ameweka wazi kuwa ushirikiano wao kwenye malezi ni mzuri.

"Diamond anasaidia sana katika malezi. Yeye hayupo karibu kila wakati lakini  huwa anatuma pesa za matumizi. Mimi ndio nalea watoto lakini yeye anasaidia sana," Zari alisema.

Mwanasoshalaiti huyo pia alifichua kwamba huwa anazuru Tanzania mara kwa mara ili watoto wake na Diamond waweze kukutana na familia.