Mjukuu wa Kibaki, Sean Andrew afunguka sababu za kunyoa dreadlocks zake

Muhtasari

•Ameeleza kuwa alichoka kubeba uzito wa nywele ndefu alizokuwa nazo na vilevile kuhusishwa na jamii ya Warasta.

•Andrew pia alifichua kuwa bado hajaweza kukabiliana na majonzi ya kifo cha marehemu babu yake ambaye aliaga Aprili 21, 2022.

Sean Andr3w
Image: Instagram

Mwanawe mfanyibiashara Jimmy Kibaki, Sean Andrew ameweka wazi kuwa alikata nywele zake kwa sababu alihitaji mabadiliko.

Mwanzoni mwa mwezi Machi, Andrew ambaye ni mmoja wa wajukuu wa aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya, hayati Mwai Kibaki aliwashangaza wengi baada ya kufichua kuwa amekata nywele zake ndefu.

Ameeleza kuwa alichoka kubeba uzito wa nywele ndefu alizokuwa nazo na vilevile kuhusishwa na jamii ya Warasta ambayo amejitenga nayo kabisa.

"Sikupenda kuitwa Ras. Sikutaka kuhusishwa na mambo hasi yanayoambatana na hilo," Andrew alifichua katika mahojiano na waandishi wa habari.

Alikuwa anazungumza wakati wa uzinduzi wa shoo halisi ya Betty Kyallo ambapo amewashirikisha dada zake. Andrew alichua kuwa alikata nywele zake katika kinyozi cha Aftershave By Flair kinachomilikiwa na mtangazaji huyo.

Alifichua kuwa mwanzoni hakuwahi kupanga kukata nywele zake kwani alikusudia kuzeeka akiwa nazo.

"Nilidhani ningezeeka nazo. Nilidhani nitakuwa na dreadlocks za kijivu lakini niliona nahitaji mabadiliko," Alisema.

Andrew pia alifichua kuwa bado hajaweza kukabiliana na majonzi ya kifo cha marehemu babu yake ambaye aliaga Aprili 21, 2022.

Alifichua kuwa ukimya wake kwenye mitandao ya kijamii umechangiwa pakubwa na hali ya kuwa bado yupo katika kipindi cha maombolezo.

"Bado naomboleza. Najaribu kuwa mwenye heshima jinsi ninavyoweza," Alisema.

Wakati wa mazishi ya hayati Kibaki yaliyofanyika Othaya, Andrew alitoa pete aliyokuwa amevaa na kuitupa ndani ya kaburi.