Mkewe Atwoli, mtangazaji Mary Kilobi azungumzia fomula ya ndoa, kupenda sababu ya pesa

Bi Kilobi alikabiliwa na maswali kadhaa kuhusiana na ndoa yao ya takribani nusu muongo.

Muhtasari

•“Waambie ndoa hainanga fomula, waende tu inakwendanga, waende vile inakwenda,” Kilobi alijibu.

•Alipoulizwa kutaja sababu kadhaa kwa nini alipendana na Bw Atwoli, alisema kwamba wakati wa kuzungumza uliopita kitambo.

Image: HISANI

Mwanahabari maarufu Mary Kilobi, ambaye pia ni mke wa bosi wa COTU Francis Atwoli alikabiliwa na maswali kadhaa kuhusiana na ndoa yao.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Bi Kilobi ambaye alionekana kusita kujibu maswali, aliombwa kufichua siri ya ndoa yao.

“Waambie ndoa hainanga fomula, waende tu inakwendanga, waende vile inakwenda,” Kilobi alijibu baada ya kuulizwa siri ya uhusiano wao.

Mtangazaji huyo alipoulizwa kutaja sababu kadhaa kwa nini alipendana na Bw Atwoli, alisema kwamba wakati wa kuzungumza uliopita kitambo.

Kilobi pia aliombwa kujibu madai ya kumpenda katibu huyo mkuu wa COTU kwa sababu ya mali yake ambapo alijibu kwa kimafumbo; “Wewe unaonaje, wewe unanijua ama hunijui? Sasa wewe ni wale ambao wanaona nilimpenda kwa sababu ya pesa. Nataka kujua wewe uko wapi?.. (mtangazaji-mimi sidhani).. sasa hilo ndilo jibu.”

Takriban miezi miwili iliyopita, Bi Kilobi (38) alimsherehekea kwa ujumbe mtamu mume wake Atwoli wakati akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 73.

Katika ujumbe wake, Kilobi alimdekeza Atwoli akisema kuwa kama ni uwezo wake angetaka asiwahi kuzeeka na badala yake aendelee kuwa mdogo na mbichi muda wote.

“Leo ni siku ya kuzaliwa ya My Prince Charming💃💃. Na ukue mdogo, ndio mdogo na mdogo zaidi kila siku Franco. Nakutakia furaha na maisha marefu sana yenye afya njema na baraka tele,” Kilobi aliandika kwenye Instagram.

Mwanahabari huyo mrembo alimtakia mume wake amani itokayo kwa Mungu pamoja na gongo lake kumfunika na kumlinda  kwani anataka kuishi naye kwa miaka mingi zaidi hadi kuzeeka pamoja.

“Mungu akulinde na kukulinda kiMungu kwa damu yake dhidi ya yule Mwovu na akupiganie vita vyako vyote vikali! Heri ya kuzaliwa Bazuu Bazenga wangu!” Kilobi alisema.

Bi Kilobi aliolewa na katibu huyo mkuu wa COTU takribani miaka 5 iliyopita ila hawajafanikiwa kupata mtoto pamoja.